Prime
Olise mchezaji wa kushangaza kuliko unavyofikiri
MICHAEL Olise nikimwona natabasamu. Mchezaji wa kushangaza kuliko unavyofikiri. Mchezaji wa maajabu. Nikimwona natabasamu tena na tena. Utashangaa mengi kuhusu kipaji chake lakini mimi huwa ananishangaza zaidi.
Amezaliwa London lakini anachezea timu ya taifa ya Ufaransa. Kwa nini? Ana mchanganyiko wa mataifa manne. Angeweza kucheza taifa lolote lile kati ya England, Nigeria, Ufaransa au Algeria. Kisa? Baba yake ni mchanganyiko wa Muingereza na Mnigeria. Ndio maana jina lake ni Olise. Jina la Kinigeria kabisa. Ni kama lile la Sunday Oliseh.
Mama yake ni Mfaransa aliyechanganya na Mualgeria. Kifupi kila mzazi wake ana uzungu na Uafrika. Inavyoonekana mama yake alimzidi nguvu baba yake. Olise hajawahi kucheza Ufaransa lakini tangu akiwa mdogo amekuwa akicheza katika timu za taifa za vijana za Ufaransa. Amezaliwa London amekulia London, lakini timu za taifa amekuwa akicheza za Ufaransa.
Wachezaji wengi huanza kucheza timu za vijana za taifa alilozaliwa. Baadae anaweza kuamua kwenda kwa mzazi mwingine. Hii haipo Afrika tu. Hata Ulaya. Hata hivyo, Olise licha ya kucheza katika timu za England pekee katika maisha yake ya soka kabla ya kwenda Bayern Munich bado aliamua kucheza zake Ufaransa. Kuanzia timu za vijana hadi sasa anapocheza timu ya wakubwa. Sijui Waingereza walimkosea nini. Au mama tu alimzidi nguvu baba.
Olise anachekesha tena pale ambapo huwa hataki kuongea na vyombo vya habari. Sio kwamba anajisikia. Hapana. Ana aibu na huwa hajui kitu cha kujibu akiulizwa maswali. Aliwahi kuulizwa na mwandishi "umefunga mabao matatu hii ina maana gani kwako" akajibu "hii ina maana ni hat trick". Amemaliza. Huwa hajui aongee nini zaidi. Badala yake ameamua awe anapiga kimya tu.
Waingereza wanamuita 'Nonchalant'. Hajali. Hana muda. Hana wasiwasi. Anajali mambo yake tu. Kuna wakati huwa namuangalia na kuamini anacheza mpira kwa sababu ana kipaji na anapata pesa. Sidhani kama anacheza kwa sababu ana mapenzi na mchezo wenyewe. Kuna wachezaji wapo hivyo. Akistaafu mpira hauoni kama anaweza kuwa mchambuzi au kocha. Ndivyo rafiki yetu Olise alivyo.
Kuna zile nyakati aliona waandishi mbele yake akageuka nyuma. Kuna wakati anafunika sura yake yote na unaweza kuhisi hajui anakokwenda. Aibu imemtawala na huwa hajui afanye nini mbele ya watu wa kawaida. Huwa anajua cha kufanya pale tu anapokabiliana na walinzi wa timu pinzani katika upande ule wa kulia.
Olise ana kichekesho kingine. Huwa anavaa viatu vya aina ya Nike. Hata hivyo, hana mkataba nao na wala hana mkataba na kampuni yoyote ya vifaa vya michezo. Kisa? Anataka kuwa huru kuvaa anachokitaka. Hataki kubanwa na mikataba. Ina maana anapoteza pesa chungu nzima kwa kuamua kuwa kama alivyo. Wala hajali.
Nyakati hizi akiwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani Olise angeweza kulipwa zaidi ya Dola 20 milioni kwa mwaka kwa ajili ya kutangaza Nike, Puma, Adidas au 'brand' nyingine yoyote kubwa duniani. Hata hivyo, anataka kuwa huru zaidi. Kina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wamekuwa wakiingiza mabilioni ya pesa kwa mikataba hii. Olise amegoma. Anataka kuwa huru.
Unamtamani Olise? Unatamani acheze katika timu yako pale England? Kama wewe ni shabiki wa Arsenal, Manchester City na Chelsea unaweza kubana meno kwa hasira ukiambiwa kuwa Olise alipita katika hizi timu. Ni kweli alipita akiwa kinda na labda walikuwa na sababu zao kutomkuza mpaka afikie kuwa mchezaji kamili.
Wengi walimwona ameibukia Crystal Palace bila ya kujua ametoka wapi. Alipita kwa wakubwa aisee. Baadaye akaibukia Reading na kisha akatua zake Palace. Kinachonishangaza ni kwa nini wakubwa wa England walimchukulia poa hadi akaenda zake Ujerumani. Ni kweli Bayern Munich wazee wa Bavaria wana pesa lakini Waingereza wana pesa nyingi kwa sasa. Na wengi wangesaidiwa na huduma za Olise.
Manchester United hawakumuona Olise? Badala yake wakaenda kwa Bryan Mbeumo. Sio mchezaji mbaya lakini leo ukiwaambia wabadilishane na Olise wa Bayern Munich watafanya hivyo kwa haraka tu bila ya kusita. Huu ni ukweli mchungu. Unaweza kubisha kwa sababu umeamua kubisha.
Manchester City? Wao waliamua kumchunia Olise bila ya kujali Bernardo Silva anaelekea mwisho wa kucheza soka katika kiwango cha juu. Hata hivyo, wanaweza kujitetea baadae waliamua kumchukua Antony Semenyo kutoka Bournemouth ambaye kwa kweli amekuwa akiwatendea haki tangu dirisha la Januari.
Arsenal wakaamua waende kwa Noni Madueke lakini wangeweza kumpata Olise kwa kiasi kile kile cha pesa ambacho walitumia kumpata Madueke. Sijui kwa nini jamaa walimchukulia poa Olise na Bayern wakaamua kupita naye. Chelsea hawaeleweki lakini Liverpool walipaswa kufanya maandalizi ya kuachana na Mo Salah kwa kumchukua Olise. Angekuwa mbadala halisi ingawa kiukweli kuna Salah mmoja tu.
Waingereza wamepuuza tu kumpata Olise. Hakuna timu ambayo angeenda kuozea benchi. Na akitoka Bayern Munich simuoni akirudi kwa Waingereza. Naweza kumuona akienda zake Hispania kucheza kwa wakubwa wa kule. Barcelona na Real Madrid. Mimi namwona kule zaidi.
Bayern Munich imeondolewa katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya hapo majuzi. Wameondolewa na PSG. Mpinzani wake katika mechi hizi mbili alikuwa Ousmane Dembele. Olise alifunga mabao yake maridhawa tu lakini mabeki wa timu yake walimuangusha. Kama angekwenda fainali na kushinda huenda angekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wangefikiriwa katika tuzo ya mwanasoka bora wa dunia.
Bahati mbaya kwake amemuachia Dembele nafasi kwa sababu Dembele anaenda kucheza na Arsenal na ana nafasi ya kushinda. Bahati mbaya nyingine aliyonayo ni mchezaji bora wa dunia anaweza pia kupatikana katika michuano ya kombe la dunia ambayo itafanyika Marekani, Canada na Mexico. Tatizo yupo timu moja na Dembele.
Kama Dembele akichukua ubingwa wa Ulaya kisha Ufaransa ikatwaa kombe la dunia basi moja kwa moja atatetea tuzo ya mwanasoka bora wa dunia ambayo aliitwaa mwaka jana. Na inashangaza mambo yalivyo sasa. Kwa nini kwa wakati mmoja Ufaransa ina Kylian Mbappe, Olise, Dembele na Rayan Cherki? Inashangaza.