Prime
Vincent Kompany na Enrique walivyoistarehesha Paris kijinga
PARIS mji wenye starehe nyingi. Mji wenye raha nyingi. Hata Princess Diana alifia katika mji huo akiwa ameenda kustarehe na rafiki yake wa kiume, Mwarabu Dodi Al Fayed. Paris ni mji wenye raha zake. Mnara wa Effel upo pale katikati ya Paris kwa ajili ya kuwapa watu starehe.
Na Jumanne usiku, Luis Enrique, kocha wa PSG pamoja na Vincent Kompany, kocha wa Bayern Munich walipeleka starehe nyingine Paris. Walipeleka mvua ya mabao katika pambano la nusu fainali la kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Matokeo yalikuwa 5-4. Kama haukutazama mechi na ghafla ukaamka asubuhi kutazama matokeo ungeweza kudhani kwamba timu zilipigiana mikwaju mitano mitano ya penalti.
Hapana haikuwa hivyo. Dunia ilishuhudia sanaa (art) moja tu ya soka. Namna ya kushambulia. Hakukuwa na sanaa yoyote ya namna ya kujihami. Kompany na Enrique wakatupa mechi yenye mabao tisa.
Lini uliwahi kuona pambano la nusu fainali Kombe la Dunia au Ligi ya Mabingwa Ulaya ama Euro au Ligi ya Mabingwa Amerika Kusini likitokea mabao tisa? Ni ngumu kutokea.
Pambano lilikuwa na sura mbili. Kuna walioona kwamba ni bonge la mechi kwa sababu ya mabao yaliyotiririka. Mfalme wa soka duniani, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele aliwahi kutuambia kuwa mpira ni mabao. Waliotazama mpira ule wa sura hii inawezekana walifurahi kwa kiasi kikubwa.
Halafu kuna kina sisi ambao tuliutazama mpira ule katika sura nyingine. Sisi ambao huwa tunatazama na kujifunza namna ambavyo timu inapaswa kuwa na sanaa ya kujihami. Hatukuambulia kitu. Sawa, Bayern Munich na PSG ni timu bora kwa sasa, lakini hata Barcelona ya Pep Guardiola ilikuwa bora na iliweza kutupa mambo yote mawili. Namna ya kuwa na mpira, namna ya kushambulia na namna ya kujihami.
Pambano la Bayern Munich na PSG hatukuona sanaa ya ukabiaji kutokea juu. Wazungu wanaita high pressing. Hatukuona sanaa ya ukabaji wa pamoja wakati adui akiwa na mpira. Na wala hatukuona sanaa ya ukabaji wa mchezaji mmoja mmoja. Wachezaji walikuwa huru sana.
Mfano ni bao la pili la Mfaransa, Michael Olise wa Bayern Munich. Aliuchukua mpira akaingia nao katikati ya boksi. Hakukuwa na mchezaji aliyeweka juhudi ya kuweka mguu wake katika kundi la wachezaji wanne wa PSG. Ukitazama upande mmoja utamsifia sana Olise. Ukitazama upande wa pili na hasa kama upo upande wa timu iliyoruhusu bao utachukia wachezaji wa timu yako.
Yalikuwepo mabao mengi ya aina hii. Bao alilofunga Khvicha Kvaratskhelia wa PSG dhidi ya Manuel Neuer nalo lilikuwa rahisi kama hivi. Akiwa anatokea kule kushoto jamaa alikuwa anatabirika ambacho anakwenda kufanya na kweli alifanya vivyo hivyo kama vile timu zilikuwa mazoezini. Ukiwa upande wa PSG utamsifia kwelikweli, lakini ukiwa upande wa timu iliyofungwa hili ni bao la kizembe kuruhusu.
Kesho yake kulikuwa na mechi ya Atletico Madrid na Arsenal. Nilijua kwamba mashabiki wangeona pambano sio tamu kwa sababu kusingekuwa na mabao mengi. Timu hizi za Diego Simeone na Mikel Arteta zingefanya sanaa zote mbili kwa pamoja. Kushambulia na kujihami. Na ndicho kilichotokea. Ilitoka sare ya 1-1 kwa mabao mawili ya penalti.
Penalti zote zilitokana na mchakato wa nidhamu ya ulinzi ya pande zote mbili. Na sasa mashabiki wengi watakuwa wapo upande wa Bayern Munich na PSG wakiamini kuwa bingwa atatoka upande ule. Sio lazima. Sio lazima sana. Wanahitaji kuwa makini kutwaa ubingwa huu. Nidhamu yao ya ulinzi lazima iimarike.
Mfano, kuna wakati PSG waliongoza kwa mabao 5-2. Sioni kama William Saliba na Gabriel Magalhaes na genge lao la wahuni linaweza kuruhusu timu itoke katika 5-2 na kufika 5-4 hasa kama pambano lenyewe ni la fainali. Wala sioni kama Simeone naye anaweza kuwa mwehu kuruhusu hilo. Wala sioni kama Jose Mourinho katika ubora wake anaweza kuruhusu hali hiyo itokee.
Kompany na Martinez inabidi wabadilike hasa. Hata katika mechi za ligi zao wamekuwa wakiruhusu mabao. Pambano la mwisho la Bundesliga Mainz walikuwa wanaongoza mabao 3-0 dhidi ya Bayern Munich lakini mwisho wa mechi Bayern alishinda mabao 4-3.
Haiwezi kutokea hivi dhidi ya Arsenal wala Atletico Madrid. Ukifungwa umefungwa. Watu wanafunga nati zao kisawasawa. Sana sana unaweza kuambulia bao moja la kufutia machozi.
Na sasa Kompany na Martinez wametuweka roho juu sisi watu wa kamari. Hatujui pambano lao la Munich litakuwaje kwa sababu hatuwaamini katika sanaa ya ulinzi. Hatujui nani anaweza kwenda Budapest pale Hungary. Wote wanaweza kufunga na wote wanaweza kufungwa muda wowote ule. Sanaa ya ushambuliaji imeizidi kwa mbali sanaa ya ukabaji. Ili timu yako iwe bora kunapaswa kuwa na uwiano katika mambo haya mawili.
Tatizo hili pia wanalo Barcelona. Wanafunga sana lakini wanafungwa sana. Hawa wakubwa wa siku hizi hawaeleweki kiurahisi ni rahisi kwao kuchana mkeka wako kwa urahisi tu. Rafiki yetu, Hans Flick huwa anakabia juu na watu wenye kasi wamekuwa wakivunja mitego ya kuotea na kuifunga Barcelona kwa urahisi tu. Haishangazi kuona leo hawapo katika hatua hii ya nusu fainali na walitolewa na Atletico Madrid.
Kompany na Martinez walipeleka starehe isiyo ya ulazima pale Paris na haishangazi kuona kila mmojawao atakuwa anajuta kwa matokeo yale. Kompany atakuwa anajiuliza, “unafungaje mabao manne, lakini bado haujashinda mechi wala kutoka sare?” Timu inayofunga mabao manne inalazimika kuwa upande wa timu ambayo imeshinda sio kupoteza mechi wala kutoa sare.
Kwa Martinez atakuwa anajiuliza, unaweza kufunga mabao matano katika pambano la nyumbani na bado usiwe na uhakika wa kufuzu katika hatua inayofuata? Bayern anahitaji mabao mawili tu aweze kufuzu moja kwa moja licha ya kufungwa mabao matano katika pambano la kwanza. Tusubiri kama kuna yeyote kati yao anaweza kubadilika pale Munich.
Kama wameamua kuistaresha dunia kwa aina hii ya mpira sawa lakini wakati mwingine huwa haifanyi kazi. Mfano rahisi ni kwamba Bayern Munich waliwahi kusafiri kwenda London kucheza na Arsenal katika hatua ya makundi. Walichapwa mabao 3-0. Kifupi ni kwamba waliruhusu mabao na hapo hapo akina Saliba na wahuni wenzake wakafanikiwa kupiga pini zao kule nyuma.
Jose Mourinho atakuwa anatazama mechi hizi huku anacheka. Anakumbuka namna ambavyo falsafa zake za ulinzi zilifanya kazi enzi zake na akawapa watu mataji ya Ulaya kwa kutumia sanaa ya ulinzi zaidi. Wakati mwingine kushambulia sio kila kitu katika soka.