Prime
Simba, Yanga ni upofu wa kushindania kivuli cha mti unaokatwa
KWA kawaida watu walio katika kada fulani huunganisha nguvu pale eneo lao linapochezewa au kutumiwa vibaya na wenye mamlaka. Watu wa kada moja huunganisha nguvu kupinga, kusifu, kuokoa n ahata kufarijiana pale penye tatizo.
Watu hao wanapoacha kushirikiana, ni rahisi kwa adui kuwatenganisha na kufanikisha mipango yake, akijua hawataunganisha nguvu kupinga kwa kuwa kila mmoja ameshika lake.
Ndivyo ilivyo kwa klabu za soka za Tanzania. Haziwezi kuungana kupinga jambo zinaloona halina masilahi kwa mpira wao au ligi yao. Upinzani wa Simba na Yanga ndio umeongeza kupumbaza viongozi, kiasi kwamba hawawezi kusimama pamoja kupigania jambo wanaloona si zuri kwa mpira.
Kibaya zaidi, wawili hawa wanafanya mambo kushindana nje ya uwanja kwa mambo ambayo pengine hayana umuhimu kwa soka letu.
Kwa matukio ya hivi karibuni tumeshuhudia ubinafsi wa wawili hao na kutofautiana katika mambo ya msingi kabisa. Kwanza, Yanga iliamua kupeleka mechi yake ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja, ikiwa ni kutotaka kujishusha baada ya kuuponda Uwanja wa Azam Complex msimu uliopita kutokana na madai walifungiwa kamera za usalama kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Lakini bado ulikuwepo Uwanja wa KMC ambao ungeweza kutumiwa kwa ajili ya mchezo huo. Na kama isingewezekana kabisa, basi mechi ingehamishiwa mikoa mingine.
Lakini Yanga ikaweka siasa mbele zaidi na kuipeleka mechi Zanzibar, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mechi ya Ligi Kuu baina ya timu hizo kuchezwa Zanzibar, ambako licha ya kuwa sehemu ya Muungano, bado kila upande una wizara yake inayosimamia masuala ya michezo.
Ndiyo ilikuwa na haki ya kuhamishia mchezo huo Zanzibar kwa kuwa Shirikisho la Soka (TFF) lilibadili kanuni na kuruhusu mechi kuchezewa Zanzibar, lakini kunatakiwa kuwepo sababu za msingi sana kuhamisha mchezo kutoka eneo ambalo klabu imeweka makao makuu yake.
Kwa wenzetu, katika kujali mashabiki wake ni vigumu kuhamishia mechi uwanja au mkoa au jimbo jingine kama hakuna tatizo nyumbani.
Ili kulipa kisasi, Simba nayo ikaamua mchezo wa marudiano ufanyika kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambao hauwezi kustahimili mvua inapokuwa kubwa.
Yanga walijaribu kupinga na kuonyesha jinsi mchezo huo unaofuatiliwa na mamilioni ya watu Afrika, utakavyopoteza mvuto na ubora wake kwa kuchezewa kwenye uwanja unaosimamisha maji na kuwa na matope.
Lakini kwa sababu ni wapinzani wa jadi, Simba waliona ni sawa tu mchezo kuchezwa hapo licha ya mvua kubwa kunyesha wakati wa kuelekea na siku ya mchezo wenyewe.
Ni mbinu za makocha tu kuamua kucheza mipira mirefu zilizonusuru mchezo huo. Kwa jumla, ile burudani iliyotakiwa kuwepo wakati wawili hao wanapokutana, ilikosa ukamilifu, huku wachezaji, hasa kipa wa Simba, wakianguka ovyo kutokana na utelezi.
Suala la uwanja na mashabiki ni vitu muhimu sana kwa mpira wa miguu. Uwanja huwezesha kandanda safi kuchezwa, wakati mashabiki huongeza nakshi na kuvuta wadhamini na ndio uhai wa klabu.
Inapofikia vinara wa soka, wakongwe wa soka au wakubwa katika soka nchini, wanatofautiana katika mambo muhimu, watawezaje kuunganisha nguvu kupigania haki za klabu? Watawezaje kupinga maamuzi mabovu ya mamlaka?
Tumeona mara kadhaa wawili hao wanashindwa kuungana na wengine kupinga maamuzi ya hovyo, kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita wakati Kamati ya Saa 72 iliposogeza kiholela muda wa kuanza mechi.
Hata TFF inaposimamisha ligi hovyo kwa sababu ya matukio ya ajabu, wawili hao wanashindwa kuunganisha nguvu kupinga kusimamisha msimu kiholela. Huona sawa tu ligi kusimama ili kuruhusu mashindano au mechi za ajabu.
Kwa Afrika Kusini, chama cha soka kikiitisha mechi nje ya tarehe za Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Ligi Kuu hukataa kusimamisha msimu na klabu haziruhusu wachezaji nyota kujiunga na timu ya taifa. Ilitokea hivyo mwaka 2011 tulipoialika Afrika Kusini kucheza mechi ya kirafiki hapa Dar es salaam. Wachezaji kama kina Tshabalala hawakuruhusiwa baada ya Ligi Kuu kuamua kuendelea na mashindano yake.
Leo hii, Simba akilalamikia uamuzi mbovu, anasimama peke yake, hali kadhalika Yanga. Hapo tuna viongozi kweli?
Matokeo yake, TFF hujifanyia maamuzi ikijua hakuna mshikamano. Inajua Yanga ikipinga, Simba itakubali na hivyo klabu jingine zitashindwa kupinga. Na kwa sababu klabu nyingi ni za taasisi za serikali, kuungana nazo kupinga uamuzi wa hovyo haiwezekani.
Simba na Yanga wanahitaji kuwa kitu kimoja katika kupigania maslahi ya klabu, katika kuhakikisha Ligi Kuu inaendeshwa kwa ubora, katika kupinga uahirishaji ovyo wa mechi, katika kupinga uamuzi mbovu na katika kupinga mgao usioendana na hali za klabu katika mikataba ya udhamini na haki za matangazo.
Simba na Yanga hazitakiwi ziendekeze upinzani wan je ya uwanja, bali ziwe kitu kimoja hadi mamlaka za soka zihofie kufanya maamuzi ya ovyo dhidi ya klabu. Zinahitaji kujua kuwa zina wajibu wa kuongoza klabu nyingine katika mambo mengi, na hasa haki zao.
Bila ya hivyo, safari ya klabu zetu itakuwa ngumu sana na ubora wao utategemea neema za Mwenyezi Mungu.