Prime
Yanga hii hizi zinatosha, Waarabu chui wa karatasi
HAIKUWEZEKANA kuondoka na pointi tatu katika Uwanja wa New Amaan Complex na wenyeji Yanga wameupachika jina la Guantanamo Bay. Ibrahim Bacca alifunga bao dakika za mwisho mwisho za kipindi cha kwanza baada ya sekeseke katika lango la Al Ahly.
Baadaye alienda kupiga saluti katika jukwaa moja la uwanja huo ambao alikuwa anauchezea kabla hajatua Yanga. Yanga wangetamani bao hilo lingekuwa pekee katika mechi hiyo lakini kipindi cha pili mechi ilikuwa tofauti na ilivyokuwa kipindi cha kwanza.
Kipindi cha kwanza Yanga walikaa na mpira kwa muda mwingi. Walitengeneza mashambulizi. Walijilinda kwa nidhamu kubwa. Walicheza vema kutokea nyuma, katikati kisha mbele. Bao la Bacca lilikuwa kama zawadi ya mashambulizi ya mara kwa mara.
Ndiyo, lilitokana na ujanja wa kuanzishiana mpira kwa haraka kati ya Pacome Zouzoua na wenzie. Bacca alikuwa katika eneo sahihi na wakati sahihi. Akaifungia Yanga bao hilo. Hata hivyo, kipindi cha pili Yanga walikuja tofauti.
Zamani Yanga walikuwa wanachanua zaidi kipindi cha pili. Pumzi yao ilikuwa inaonekana kubwa zaidi kipindi cha pili kiasi kwamba watani zao wakaanza kuwazushia huenda walikuwa wanatumia dawa za kuongeza nguvu.
Hata hivyo, Yanga ya jana ilikuwa tofauti. Kipindi cha pili ilikata moto na kuzua taharuki kwa mashabiki wao. Na ni hapo ndipo Aliou Dieng, staa wa kimataifa wa Mali alipopata nafasi ya kumtungua kipa wake wa timu ya taifa, Djigui Diara. Lilikuwa bao kama la Bacca ambalo lilitokana na sekeseke katika lango la mpinzani.
Hakukuwa na jipya tena baada ya bao la Dieng sana sana Al Ahly walionekana kumiliki mpira zaidi kuliko Yanga. Mpira ulipoisha Yanga walijikuta na pointi tano huku wakiwa na mechi mbili mkononi. Ni katika kundi ambalo lilitajwa kuwa la kifo kwao. Alipangwa na Waarabu watupu.
Baada ya mechi Al Ahly alijikuta anaongoza kundi kwa pointi nane. Baadaye usiku ilichezwa mechi kati ya watu wengine wawili katika kundi. FAR Rabat na JS Kabylie ya Algeria. Ulikuwa mchezo ambao haukuwa na mvuto na FAR Rabat walikuwa wanacheza nyumbani bila ya mashabiki.
Yanga walipenda pambano hili liishe kwa sare kama lile la mwanzo lakini kipindi cha pili dakika za jioni wenyeji walipata bao ambalo liliwapeleka katika pointi tano kama za Yanga. Kuna jambo ambalo nimelitafakari kwa kina.
Kuna uwezekano mkubwa Yanga wakavuka kundi lao. Sijaona maajabu makubwa kutoka kwa FAR Rabat na tayari Yanga wamemaliza mechi zao mbili ngumu dhidi ya timu ngumu zaidi katika kundi, Al Ahly. FAR Rabat ambao walifungwa Unguja na Yanga sio wagumu kuliko Al Ahly. Na wanatakapocheza bila ya mashabiki kwa mara nyingine tena pale Rabat maisha yatakuwa rahisi kwa Yanga.
Yanga atahitaji sare tu katika pambano hilo kabla ya kufunga kazi kwa kumfunga kibonde wa kundi JS Kabylie pale Unguja. Na kuna uwezekano pia Yanga wakapata matokeo mazuri zaidi ya sare pale Morocco. Yanga hii inayotengenezwa upya kwa uwepo wa kina Alan Okello, Depu, Pacome, Max, Duke Abuya, Camara Domaro na wengineo inaweza kufanya jambo Rabat. Hakuna ambacho kitashangaza.
Nalisema hili huku pia nikiutafakari mpira wenyewe wa Afrika. Kama Yanga wakipenya katika kundi lao wanaweza kushikiwa mbali zaidi katika hatua kama ya nusu fainali. Siku moja kabla ya mechi hii nilikuwa natazama pambano la Mamelodi Sundowns na Al Hilal ya Sudan. Mamelodi walichapwa 2-1.
Kiukweli kabisa klabu nyingi kubwa za Afrika zinacheza mpira wa kawaida tu. kuanzia Al Ahly yenyewe hadi hawa kina Mamelodi. Sijawaona mabingwa watetezi Pyramids lakini hawa kina Al Ahly sio wale kina Mohamed Barakat au Aboutrika. Sio wale kina Flavio. Sio wale kina Hossam Hassan.
Wanacheza mpira mzuri wa kawaida tu ambao haujanishangaza kwa nini Pyramids alikuwa bingwa wetu msimu uliopita. Hawachezi katika staili ile ambayo walikuwa wanapambana na TP Mazembe ya kina Mbwana Samatta na Tresor Mputu.
Sijui kama sisi tumesogea kidogo au wao wameshuka kidogo lakini ukweli ni hawashtui. Inanipa kiburi kusema Yanga akipenya hapa anaweza kwenda mbali zaidi. Na inanipa kiburi kusema kama hali hii ingekutana na Simba ile ya kina Jose Louis Miquissone, Clatous Chama na John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu huenda ingefika hadi fainali.
Kuna kitu hakipo sawa sana kwa wakubwa, hasa wale wa Afrika Kaskazini. Wamekuwa chui wa karatasi. Wakati huo huo Pedro Concalves akichanga karata zake vyema huenda Yanga ikafika mbali. Ubora upo, pia ana machaguo mengi mazuri ndani ya uwanja na nje ya uwanja.
Wakati mwingine nadhani machaguo haya yanamchanganya. Kwa mfano, katika mechi ya jana ambayo ilihitaji utulivu mwingi wa kukaa na mpira, Chadrack Boka alipaswa kuanzia nje na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ angeanza. Boka ndiye aliyeigharimu Yanga bao la wageni. Angeweza kuwa bora zaidi.
Vyovyote ilivyo nafasi ya Yanga ipo. Zamani ingekuwa kiama kupangwa na Waarabu watatu katika kundi moja. Waarabu kutoka Misri, Algeria na Morocco. Kwa sasa sio dhambi kubwa na tunavyozungumza Yanga inashika nafasi ya pili katika kundi.
Kesho tutamwangalia mtani wa Yanga Mnyama ambaye alitarajiwa kucheza na Esperance katika siku ambayo Mnyama anaipenda zaidi, leoJumapili.