Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gamondi aachwe afanye kazi kwa utulivu

GAMONDI Pict

Muktasari:

  • Gamondi anayeinoa Singida Black Stars, ameteuliwa katika kipindi nyeti na cha matumaini makubwa kwa watanzania wote wapenzi wa soka. Wakati huu ambapo macho ya mashabiki, wanahabari na wadau wa michezo yameelekezwa kwake.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefanya uteuzi wa kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars, Miguel Gamondi, kuchukua nafasi ya aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Gamondi anayeinoa Singida Black Stars, ameteuliwa katika kipindi nyeti na cha matumaini makubwa kwa watanzania wote wapenzi wa soka. Wakati huu ambapo macho ya mashabiki, wanahabari na wadau wa michezo yameelekezwa kwake.

Kocha huyo sio mgeni katika soka la Afrika. Ni kocha mwenye uzoefu katika ligi mbalimbali barani humo, akijulikana kwa nidhamu, falsafa ya soka la kushambulia, na uwezo wa kukuza vipaji chipukizi.

Kuteuliwa kwake kuinoa Taifa Stars kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika Morocco ni ishara kwamba TFF, ina nia ya kujenga timu imara, yenye ushindani, na inayoweza kuleta matokeo chanya.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayoikabili Tanzania si uwezo wa makocha pekee, bali presha na maneno kutoka kwa mashabiki na wadau ambao mara nyingi hupenda kutoa maoni kabla hata ya matokeo kuonekana.

Ni kawaida kuona mitandao ya kijamii ikifurika lawama au kejeli kila timu inapoteuliwa au kufanya vibaya, bila kutazama sababu za msingi kama maandalizi duni, muda mfupi wa kocha na wachezaji au mazingira magumu ya michuano.

Tunapaswa kutambua kazi ya Gamondi si ndogo. Anakabidhiwa jukumu la kujenga timu yenye umoja na ubora wa kimataifa, kuandaa mikakati sahihi ya ushindani, na kuwafanya wachezaji waamini katika uwezo wao. Ili hayo yote yawezekane, anahitaji kitu kimoja muhimu kutoka kwa watanzania, ushirikiano na uvumilivu.

Mashabiki wana mchango mkubwa katika mafanikio ya timu. Badala ya kumhukumu mapema au kumtupia lawama, ni bora kumtia moyo na kumuunga mkono kwa vitendo. Hii inamaanisha kujitokeza kwa wingi viwanjani, kuhamasisha amani na nidhamu miongoni mwa wachezaji, na kutoa maoni ya kujenga badala ya kubeza.

TFF na wadau wengine wanapaswa kumwezesha Gamondi kwa kila anachohitaji, kuanzia maandalizi bora, mechi za kirafiki za kiwango cha juu hadi mazingira mazuri ya kazi. Bila sapoti ya kweli kutoka kwa mfumo mzima wa michezo nchini, hata kocha bora duniani hatapata mafanikio.

Afcon 2025 si ndoto isiyowezekana. Tanzania imeonyesha dalili za maendeleo katika miaka ya karibuni, ikishiriki michuano mikubwa na kutoa wachezaji wanaotamba ndani na nje ya nchi. Hivyo basi, kinachohitajika sasa ni kuendeleza msingi huo kwa umoja na mtazamo chanya.

Kwa maneno mengine, uteuzi wake usiende na maneno ya kukatisha tamaa au mashindano ya nani anajua zaidi ya mwingine, bali ni wakati wa kuwa wamoja, kumuamini Gamondi na kuiunga mkono bila ya mashaka.

Tukifanya hivyo, hakika tutashuhudia matokeo makubwa si tu Afcon 2025, bali katika mustakabali mzima wa soka la Tanzania kama tulivyoshuhudia chini ya Morocco wakati akiinoa timu hiyo kwa ilichokifanya katika CHAN 2024 kwa kufika robo fainali. Tumpeni Gamondi nafasi, tumpeni muda na tumpe imani. Taifa Stars ni yetu sote.