Serengeti Girls isikate tamaa, nafasi ipo
Muktasari:
- Katika mechi hiyo Serengeti Girls ilikubaki kipigio cha mabao 2-0 na hivyo kusubiri ile ya marudiano itakayopigwa Afrika Kusini kujaribu bahati yao ya kufuzu fainali hizo zitakazofanyika Morocco Oktoba 17 hadi Novemba 7 mwaka huu 2026.
JUZI Jumamosi, timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17 ilicheza dhidi ya Afrika Kusini mechi ya kwanza wa raundi ya pili ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 17.
Katika mechi hiyo Serengeti Girls ilikubaki kipigio cha mabao 2-0 na hivyo kusubiri ile ya marudiano itakayopigwa Afrika Kusini kujaribu bahati yao ya kufuzu fainali hizo zitakazofanyika Morocco Oktoba 17 hadi Novemba 7 mwaka huu 2026.
Hata hivyo, kipigo ilichopata hakipaswi kuwa mwisho wa ndoto zao na badala yake, kiwe somo na hamasa ya kupambana zaidi katika mechi wa marudiano.
Ni kweli matokeo hayo yanaweka kazi kubwa mbele yao, lakini katika soka hakuna lisilowezekana. Serengeti Girls bado ina nafasi ya kurejea na kubadilisha hali ikiwa itaingia katika mechi hiyo ikiamini inaweza.
Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Morocco ni ndoto kubwa kwa soka la wanawake Tanzania na ndiyo maana hakuna sababu ya kukata tamaa mapema wakati nafasi bado ipo.
Kikubwa kilichoonekana katika mechi ya kwanza ni ukosefu wa umakini katika kutumia nafasi walizozipata pamoja na makosa ya safu ya ulinzi yaliyoigharimu timu. Haya ni mambo ambayo benchi la ufundi linapaswa kuyafanyia kazi haraka kabla ya mechi ya marudiano. Katika hatua kama hizi, makosa madogo yanaweza kuamua hatma ya timu.
Pia, wachezaji wanapaswa kuondoa presha ya matokeo ya kwanza na kucheza kwa kujiamini. Soka la vijana linahitaji ujasiri, nidhamu na moyo wa kupambana hadi dakika ya mwisho. Serengeti Girls wana uwezo wa kufanya vizuri ikiwa wataamini katika uwezo wao.
Watanzania bado wana sababu ya kuwaamini vijana hawa. Kumbukumbu ya mwaka 2022 bado ipo wazi baada ya Serengeti Girls kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika India na kufika hatua ya robo fainali. Mafanikio yale yalitokana na ubora wao na sasa ni wakati wa kujipanga kwa ajili ya kwenda Afrika kusini kupindua matokeo.
Ndiyo maana kikosi hiki cha sasa kinapaswa kutumia historia hiyo kama nguvu ya kuongeza morali. Wamebeba ndoto za taifa na wana nafasi ya kuandika historia nyingine kubwa ikiwa wataonyesha moyo wa ushindi katika mechi ya marudiano.
Kilichobaki sasa ni maandalizi chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime, umakini mkubwa na matumizi sahihi ya nafasi watakazozipata. Wachezaji wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa huku benchi la ufundi likihakikisha timu inaingia uwanjani ikiwa tayari kupambana kwa nguvu zote.
Ni wazi nafasi hiyo wanayo kinachotakiwa sasa ni kupambana hadi mwisho kwa ajili ya ndoto ya kurejea tena Kombe la Dunia.