KVZ bingwa Ngao ya Jamii Zanzibar ikiichapa KMKM
Muktasari:
- Mechi hiyo imechezwa leo Agosti 23, 2026 saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Mao Zedong, Unguja.
TIMU ya KVZ, imeibuka bingwa wa Ngao ya Jamii Zanzibar kwa kuifunga KMKM penalti 8-7 baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo kufungana mabao 2-2.
Mechi hiyo imechezwa leo Agosti 23, 2026 saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Mao Zedong, Unguja.
Jusper Babalika aliitanguliza KMKM kwa kufunga bao la kwanza dakika ya 14. Kuingia kwa bao hilo, KVZ ikalazimika kufanya mabadiliko ya haraka, lakini hata hivyo, hadi mapumziko, KMKM ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Dakika ya 52, KMKM ikapata bao la pili likifungwa na Matheo Antony kwa mkwaju wa penalti. Matumaini ya KMKM kutetea Ngao ya Jamii yalikuwa makubwa kabla ya mambo kubadilika.
KVZ ilijipanga upya na kusawazisha mabao hayo yakifungwa na Mudrik Gonda na Akram Muhina 'Haland' na kupeleka mchezo hatua ya mikwaju ya penalti ambapo kila upande ukipiga tisa, KVZ ikifunga nane na kukosa moja, wakati KMKM ikikosa mbili, ikifunga saba.
Katika penalti tano za kwanza, kila upande ulikosa moja, kisha baadaye kwenye piga nikupige, ndipo KMKM ikakosa pigo la tisa na kuipa ushindi KVZ.
Timu ya KMKM imeshindwa kutetea Ngao ya Jamii iliyoshinda msimu wa 2025-2026 baada ya kuifunga Mlandege penalti 5-3 baada ya dakika 90 kutoka 0-0.
Kumalizika kwa mechi hiyo, kunafungua rasmi msimu wa soka Zanzibar 2026-2027 ambapo Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Agosti 29, 2026.