Prime
Magori afungua mkoba, ataka chuma cha kigeni
KAMA Simba itakosa ubingwa msimu huu moja ya sababu itakuwa ni kosa mshambuliaji kinara, katika kuliepuka hilo uongozi wa miamba hiyo umedhamilia kutumia dirisha hili la usajili kusajili straika mabao.
Mastraika wawili wa Simba msimu huu hadi sasa wamefunga mabao 11 tu ambao Selemani Mwalimu mabao nane huku Mghana Jonathan Sowah matatu kabla ya kuingia katika matatizo yake na uongozi na sasa ameondoka kambini.
Kukosa ufanisi kwa washambuliaji hao kunamlazimisha kocha Steve Barker kuwatumia Elie Mpanzu aliyefunga mabao manne na Inno Loemba kama washambuliaji kivuli huku mabao mengi yakifungwa na viungo Clatous Chama (mabao 8), Libase Gueye (6) na Anciet Oura (4) kati ya mabao 45 iliyofunga timu hiyo hadi sasa kati ligi kuu.
Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikioendelea kufukuzana na Yanga ambayo inaongoza kwa tofauti ya pointi mbili timu zote zikisalia na mechi tano kumaliza msimu na wekundu hao bado wanaamini wana safari ya kukiimarisha kikosi hicho.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa bodi ya Simba, Crescentius Magori amefunguka licha ya timu hiyo kuendelea kufukuzia mataji, lakini msimu huu ukimalizika, watakwenda kukiimarisha zaidi kikosi hicho katika safu ya ushambuliaji.
Simba msimu huu ilitangaza bajeti ya Sh 29.5 Bilioni hivyo haitokuwa tatizo kuwa kuvunja benki na kumnunua mshambuliaji mwenye ubora utakaowasaidia katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Magori amesema watakuwa watulivu kutafuta mshambulaiji bora zaidi ambaye atakuja kuongeza nguvu katika kikosi hicho tayari kwa mapambano ya msimu ujao eneo ambalo wamelifanyia tathimini ya kina.
“Tunajipanga ligi ikiisha tutajaribu kukiboresha kikosi chetu ili kiwe imara zaidi kuliko hiki cha sasa, kazi imeshaanza ya kuboresha kikosi, naomba niiseme kwa sasa ripoti ya kocha lakini kazi imeshaanza na tunaendelea,” amesema Magori ambaye jana alifanya ziara kwenye kampuni inayotengeneza gazeti hili.
“Kuna mambo mawili kuna kundi la wachezaji wa kigeni bado tunafanyia kazi kwa sababu tunataka kuleta wachezaji wazuri zaidi ambao wataongeza nguvu zaidi ya hapa tulipofikia kwenye timu yetu ya sasa.
“Tunatafuta straika tunaamini tunakwenda kutafuta mtu bora kuliko tulionao sasa, hilo ni eneo ambalo lipo linafanya vizuri, lakini tunaamini ingeweza kufanya vizuri zaidi kama tungekuwa na watu bora zaidi.
Miongoni wa washambuliaji wanaowania na Simba ni Souleymane Fofana mfungaji bora ASEC Mimosas aliyefunga mabao 14 katika ligi ya Ivory Coast, mbali ya huyo pia yupo Kevin Bakare pamoja na nyota wengine kutoka Afrika Kusini anapotokea kocha Barker.
Katika eneo la kiungo pia wapo ambao wanafanya vizuri, lakini tunataka walio bora zaidi ili kuiongezea timu nguvu tunayoikusudia.”
Mpaka sasa Simba kuna wachezaji wawili wanaofanya vizuri katika kufungaji wakilingana ambao ni mshambuliaji Seleman Mwalimu na kiungo Chama ambao wote wamefunga mabao nane kila mmoja.
Simba msimu huu haikufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa baada ya kumaliza wakiwa wa mwisho katika kundi lake alilokuwa pamoja na Esperance (Tunisia), Petro Atletico de Luanda (Angola) na Stade Malien ya Mali.
Aidha Magori akizungumzia wachezaji wazawa amethibitisha timu hiyo imeshafanikiwa kupata baadhi ya wachezaji wa ndani ambao itamalizana nao tayari kwa msimu ujao, huku akificha kuwataja kwa majina.
Kuna wachezaji wa ndani tayari tunao, tupo kwenye mipango ya kumalizana nao, wakati ukifika tutawajulisha na kazi hiyo pia inaendelea lengo letu ni kwamba mambo haya ya usajili tuyamalize mapema.”
Hata hivyo taarifa zinadai miamba hiyo ya Msimbazi tayari wamefikia makubaliano na kiungo wa Pamba, Kelvin Nashon pamoja na winga wa TRA United, Ramadhan Chobwedo ili wajiunga nao.