Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzani uko sawa Dabi ya Kariakoo

ISAMUHYO

Muktasari:

  • Simba imeweka rekodi na kuwa  timu ya kwanza msimu huu kuifunga Yanga mabao mawili ndani ya dakika kumi baada ya kutawala dakika za mwanzoni za mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wa wastani.

Dakika tisini za mchezo wa Simba na Yanga zimeonyesha kuwa mzani umebalansi hadi sasa msimu huu, baada ya mechi ya Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, katika mechi ngumu iliyopigwa Uwanja wa Meja Isamuhyo.

Simba imeweka rekodi na kuwa  timu ya kwanza msimu huu kuifunga Yanga mabao mawili ndani ya dakika kumi baada ya kutawala dakika za mwanzoni za mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wa wastani.

Hii ni mechi ya pili timu hizo zinatoka sare msimu huu wa ligi baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza  kumalizika kwa suluhu, hata hivyo, siku nne zilizopita Simba iliichapa Yanga bao 1-0 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano ikiwa ni mara ya kwanza inatwaa ubingwa huo baada ya kupita miaka miwili.

ISAMU 04

Simba ambayo ilianza mchezo wa jana, bila mshambuliaji asilia baada ya Seleman Mwalimu kuanzia benchi iliwahitaji dakika mbili tu kufanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Libase Gueye ambaye alipata pasi safi kutokana na kiungo mahiri wa timu hiyo Clatous Chama na kufunga kwa ufundi wa hali ya juu.

ISAMU 01

Baada ya bao hilo, Simba iliendelea kutawala kwenye mchezo huo kwa kupiga pasi fupi za haraka na kuonekana kuwachanganya zaidi Yanga, kama kuna kitu kitabaki kumbukumbu kwenye soka la Tanzania basi ni bao safi ambalo liliwekwa kimiani na Chama katika dakika ya tisa ya mchezo akipata pasi safi kutoka kwa Ellie Mpanzu Kibisawala.

Hili linaweza kuwa bao bora la msimu huu kutokana na ustadi aliouonyesha Chama likiwa ni la nne kwake kwenye ligi msimu huu.

Pamoja na eneo la kuchezea la Uwanja wa Meja Isamuhyo kutokuwa kwenye mazingira mazuri ya kucheza soka la kuvutia kutokana na mvua ambazo zimekuwa zikiendelea kunyesha jijini Dar es Salaam, Maxi Nzengeli alipiga krosi safi katika dakika ya 17 ambapo beki wa Simba Ismael Toure, aliokoa mpira huo kizembe ambapo ulimkuta Prince Dube na kuifungia timu yao bao safi na kuwapeleka Wananchi mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao 2-1, hili ni bao la tisa kwa Dube kwenye ligi akiwa sawa na Feisal Salum 'Fei Toto' wote wakiwa kileleni kwenye chati ya ufungaji.

ISAMU 02

Kipindi cha pili, Yanga ilifanya mabadiliko na kumtoa Israel Mwenda na nafasi yake kuchukuliwa na Yao Atohoula huku Aurelio Depu akiingia kuchukua nafasi ya Damaro ambaye tayari alikuwa na kadi ya njano.

Kuingia kwa mastaa hao kuliibadilisha Yanga na kuanza kutawala mchezo huo ambapo dakika ya 51, Bakari Nondo Mwamnyeto aliisawazishia Yanga baada ya mabeki wa timu hiyo kushindwa kuokoa mpira uliokuwa ukizagaa langoni mwao.

ISAMU 05

Dakika ya 25 za mwisho timu hizo zilionekana kushambuliana kwa zamu huku Yanga wakipoteza nafasi za wazi kupitia kwa Dube ambaye alibaki mwenyewe na kipa na kupiga mpira nje, huku upande wa Simba wakipoteza nafasi ya bao kupitia kwa Gueye ambaye alionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo huo.

ISAMU 03

Sare hiyo imeifanya Yanga kufikisha michezo 40 bila kupoteza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu hadi sasa na hivyo bado utawala wao unaendelea, ikiwa mara ya mwisho ilipoteza msimu uliopita ilipochapwa mabao 3-1 na Tabora United.

Hata hivyo kuonyesha kuwa mzani umebalansi msimu huu, katika mchezo wa Ngao ya Jamii Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Simba ikashinda bao 1-0 kwenye Muungano, lakini mechi zote za ligi zimemalizika kwa sare ikiwa ni mara ya kwanza kwa kipindi cha hivi karibuni timu hiyo kutoka sare kwenye michezo yote miwili ya ligi Kuu Bara, labda mbabe atapatikana kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB

Yanga imeendelea kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imefikisha pointi 48 baada ya kucheza michezo 20, huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 43, zote zikiwa kwenye mbio za ubingwa.

ISAMU 06

YANGA YATUMIA MJENGO WA KIFAHARI

Katika hali ambayo ilikuwa haijatarajiwi na wengi kikosi cha Yanga jana kiligoma kutumia vyumba vya kubadilishia nguo na kutumia nyumba ya jirani na Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Nyumba hiyo iliyotumika ni ya  kifahari yenye rangi nyeupe inayong’aa, likiwa limezungukwa na fensi yenye nyaya za umeme juu yake ilitumiwa na mastaa hao mara tu baada ya kufika uwanjani hapo.

Nyumba hiyo ambayo inatazamana na geti kuu la uwanja huo,  iligeuka kuwa sehemu ya maandalizi ya timu hiyo.

ISAMU 07

Awali, Simba walikuwa wa kwanza kuwasili uwanjani, wakionyesha utulivu mkubwa saa 10:25 jioni, dakika 20 baadaye ndipo msafara wa Yanga uliwasili lakini ukaingia katika sintofahamu ya muda mfupi.

Katika hekaheka hiyo kulikuwa na mkanganyiko katika uratibu wa kuingiza timu hiyo uwanjani huku baadhi ya maofisa wa usalama ikiwemo makomandoo wakionekana kufunga njia kwa muda.

Msongamano ulijitokeza kwa muda mfupi katika geti kuu, ndipo Yanga walipoelekea kwenye  nyumba nyeupe ya jirani, wakiingia kwa uharaka, wakitumia eneo hilo kama sehemu ya kujipanga kwa mechi hiyo.