Simba, Yanga zabisha hodi TFF
Muktasari:
- Stars iko katika ratiba ya mechi ya kirafiki kalenda ya FIFA, ikijipanga kuvaana na Kuwait, Novemba 14, jijini Cairo, Misri na kulikuwa na mpango wa kucheza mechi ya pili dhidi ya Algeria ambayo imefutwa kabla haijatangazwa.
TAIFA Stars itacheza mechi moja dhidi ya Kuwait, baada ya viongozi wa klabu za Simba na Yanga kugonga hodi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba mastaa wanaoshiriki michuano ya CAF kurejea katika vikosi vyao mapema.
Stars iko katika ratiba ya mechi ya kirafiki kalenda ya FIFA, ikijipanga kuvaana na Kuwait, Novemba 14, jijini Cairo, Misri na kulikuwa na mpango wa kucheza mechi ya pili dhidi ya Algeria ambayo imefutwa kabla haijatangazwa.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, mechi zilikuwa zipigwe mbili, ila kuna maombi yalitumwa na Simba na Yanga ili wachezaji wanaochezea timu zinazoshiriki makundi warudi mapema ili kupata wasaa wa kujiunga na wenzao kambini.
“Mmoja kati ya aliyetuma ombi hilo ni kiongozi kutoka Yanga, lakini ratiba ilikuwa inasoma Stars icheze na Algeria, huko Misri.
“Ratiba hiyo ilitokana na mechi dhidi ya Kuwait iliyopangwa kuchezwa Misri, lakini walipofika huko walikuta Misri inacheza na Algeria. Hivyo wakaomba kucheza na Algeria, lakini wakati wanasubiri majibu, huku maombi ya kuomba mastaa kuwahi kurejea yakawa yamefika mlangoni kutokana na uwepo wa mechi za CAF, ndio maana mchezo umebaki mmoja.”
Mwanaspoti lilimsaka Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo na amesema kwa sasa Stars itacheza mechi moja kama ratiba ilivyo.
“Ni kweli tumekuwa na ratiba ya kucheza mechi zaidi ya moja, lakini mambo yamebadilika kidogo ila mwanzo ilipangwa Stars icheze michezo miwili. Timu tuliyopanga kucheza nayo, ratiba kwa upande wao ilikuwa imebana hivyo haikuwezekana kupata muda wa mchezo huo,” amesema ndimbo na kuongeza; “Hii itakuwa ni fursa pia kwa wachezaji wanaoshiriki michuano ya CAF, kujiunga na timu zao kwa wakati.”
Ikumbukwe, Simba na Yanga zinajiandaa kucheza makundi Ligi ya Mabingwa, huku Azam FC na Singida Black Stars zikijipanga na Kombe la Shirikisho Afrika. Yanga itaanza kuvaana na FAR Rabat ya Morocco wakati Simb itaikaribisha Petro Atletico ya Angola.