Tanzanite Queens yapewa Brazil, England Kombe la Dunia Wanawake U-20
Muktasari:
- Droo hiyo imechezeshwa leo Mei 15, 2026 katika mji wa Łódź nchini Poland ambapo fainali hizo zitafanyika kuanzia Septemba 5, 2026 hadi Septemba 27, 2026 ikishirikisha timu 24.
UPANGAJI wa makundi na ratiba kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20, umeifanya Tanzanite Queens kuangukia Kundi B lenye timu za Brazil, England na Canada.
Droo hiyo imechezeshwa leo Mei 15, 2026 katika mji wa Łódź nchini Poland ambapo fainali hizo zitafanyika kuanzia Septemba 5, 2026 hadi Septemba 27, 2026 ikishirikisha timu 24.
Baada ya kupangwa makundi hayo yenye timu nne, Tanzanite Queens ambayo ni Timu ya Soka ya Wanawake Tanzania chini ya miaka 20, mechi ya kwanza itakuwa Septemba 5, 2026 dhidi ya Brazil, kisha Septemba 8, 2026 itaikabili England, kisha itamalizana na Canada Septemba 11, 2026.
Timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kutoka makundi sita, zitafuzu hatua ya 16 bora, zikiungana na 12 zitakazomaliza nafasi mbili za juu katika makundi yote.
Afrika ambapo imeingiza timu nne katika fainali hizo, mbali na Tanzania, zingine ni Nigeria, Ghana na Benin.
Hii ni mara ya kwanza Tanzania kushiriki Kombe la Dunia Wanawake kwa umri huo sambamba na Benin, Poland, Ureno na Ecuador.
Kwa Afrika ukiziweka kando Tanzania na Benin, Ghana inakwenda kushiriki mara ya nane baada ya mwaka 2010, 2012, 2014, 2016, 2018, 2022, 2024, huku Nigeria ikifuzu mara 12 (2002, 2004, 2006, 2008, 2010, 2012, 2014, 2016, 2018, 2022, 2024 na sasa 2026.
Safari ya Tanzanite Queens kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu ilianzia raundi ya pili baada ya kuitoa Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0, ikishinda mabao 4-0 katika mechi ya kwanza na marudiano 3-0.
Raundi ya tatu ikaitoa Kenya kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na raundi ya nne ikakutana na Cameroon.
Mechi ya kwanza raundi ya nne, Tanzanite Queens ilipoteza ugenini kwa mabao 3-1 kule Cameroon, lakini ikashinda nyumbani 2-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kuifanya ifuzu Kombe la Dunia kwa faida ya bao la ugenini kufuatia matokeo ya jumla kuwa 3-3.
MAKUNDI
Kundi A: Poland, Argentina, Mexico, Benin
Kundi B: Brazil, Tanzania, Canada, England
Kundi C: Ufaransa, Korea Kusini, Ecuador, Ghana
Kundi D: Japan, New Zealand, Marekani, Italia
Kundi E: Korea Kaskazini, Ureno, Costa Rica, Colombia
Kundi F: Hispania, Nigeria, New Caledonia, China
RATIBA KUNDI B
Septemba 5, 2026
Brazil v Tanzania (Saa 9:00 alasiri)
Canada v England (Saa 12:00 jioni)
Septemba 8, 2026
Brazil v Canada (Saa 9:00 alasiri)
England v Tanzania (Saa 12:00 jioni)
Septemba 11, 2026
England v Brazil (Saa 9:00 alasiri)
Tanzania v Canada (Saa 9:00 alasiri)