Prime
Winga huyu alivyochomolewa Ulaya hadi Msimbazi
UHAMISHO wa winga, Anicet Oura kujiunga na wekundu wa Msimbazi, Simba katika dirisha hili la usajili haukuwa wa kubahatisha hata kidogo. Unaambiwa ulikuwa ni uamuzi wa kimkakati uliozingatia maslahi ya sasa na baadaye ya mchezaji huyo.
Hayo yameelezwa na wakala wake, Serkan Dag wa Mountain Sports Management aliyekuwa nchini kutokea Ubelgiji, katika mazungumzo yake na Mwanaspoti, aliyefichua kuwa mazungumzo kati ya Simba na upande wa mchezaji yalifanyika kwa uwazi hali iliyochochea dili hilo kukamilika ndani ya wiki moja tu.
“Katika mazungumzo hayo hakukuwa na changamoto yoyote, pande zote zilikuwa wazi, Simba iliwasilisha ofa yao (nono), nasi tuliwasilisha mahitaji yetu, uwepo wa kocha wake wa zamani, Steven (Barker), ulikuwa sababu muhimu katika kukamilika kwa uhamisho huu,” amesema Serkan.
Wakala huyo ameisifu menejimenti ya Simba pamoja na rais wa heshima wa klabu hiyo na mwekezaji, Mohammed Dewji akieleza walionesha ukarimu, uaminifu na nia ya kweli tangu mwanzo wa mazungumzo.
“Uongozi wa Simba na rais wake walikuwa wakarimu na wa kweli, walionesha nia ya dhati kabisa, ni watu wazuri sana kufanya nao kazi,”€ aliongeza.
Licha ya Simba kufanikiwa kuinasa saini ya Oura, Serkan alifichua kuwa mchezaji huyo alikuwa na ofa nyingine kadhaa, zikiwamo kutoka klabu za Finland, Uturuki na Ukraine.
Amesema kabla ya kujiunga na Simba, Oura alikuwa kambini kwa wiki mbili Antalya, Uturuki na klabu moja ya Ukraine, lakini upande wa mchezaji ulisita kusaini mara moja kutokana na hali ya vita nchini humo.
“Kulikuwa pia na ofa iliyoboreshwa kutoka klabu ya Finland na klabu moja ya Uturuki, tulizipitia ofa zote tukazungumza na mchezaji, tukafanya uamuzi kwa pamoja uamuzi wetu wa mwisho tuliichagua Simba na tunaamini ulikuwa uamuzi sahihi,” amesema.
Kwa mujibu wa wakala huyo, uhamisho wa Oura kwenda Simba haupaswi kutazamwa kama kurejea tu barani Afrika, bali ni hatua ya kimkakati katika kujenga upya na kuinua thamani ya mchezaji huyo.
“Simba si klabu ya kawaida ya ndani ni chapa kubwa barani Afrika, inayoshiriki mara kwa mara mashindano ya CAF, jambo linalowapa wachezaji mwonekano mkubwa kimataifa,” amesema Serkan.
Juzi, Oura aliichezea Simba mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mashujaa FC, ambapo baada ya mchezo huo alieleza furaha yake kutua Msimbazi.
“Ninafuraha kuwa hapa, malengo yangu ni kufanya vizuri na kuhakikisha mashabiki wanafurahia uwepo wangu, najua ukubwa wa Simba na ugumu wa kazi iliyopo mbele,” amesema Oura.
Usajili wa Oura Simba pamoja na mastaa wengine ambao wametua katika dirisha hilo dogo, akiwemo Libasse Gueye ambaye alipachika bao la kwanza la Simba dhidi ya Mashujaa, umebeba matumani mapya ya timu hiyo ambayo jana ilicheza mechi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuikaribisha Esperance Sportive de Tunis kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kundi D kufuatia kupoteza mechi tatu za kwanza mfululizo.