Anthony Gordon atua katika anga za Bayern Munich
Muktasari:
- Hata hivyo, Newcastle imeweka wazi kuwa haiwezi kumwachia kirahisi nyota huyo na inataka dau linalokaribia Pauni 80 milioni ili kuanza mazungumzo ya uhamisho.
BAYERN Munich imeonyesha nia ya dhati ya kumsajili winga wa Newcastle United na England, Anthony Gordon, 25, katika dirisha lijalo la kiangazi.
Hata hivyo, Newcastle imeweka wazi kuwa haiwezi kumwachia kirahisi nyota huyo na inataka dau linalokaribia Pauni 80 milioni ili kuanza mazungumzo ya uhamisho.
Gordon ameendelea kuwa katika rada za timu nyingi kwa muda mrefu, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kiasi cha pesa kinachohitajika na Newcastle ili kumuuza.
Awali, ilielezwa kwamba timu hiyo inataka zaidi ya Pauni 90 milioni ili kumuuza mchezaji huyo ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 46 za michuano yote na kufunga mabao 17.
Iwapo Bayern Munich itafikia kiwango hicho cha fedha dili linaweza kuwa moja ya usajili mkubwa wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo, kipaumbele cha kwanza cha Newcastle ni kuhakikisha inambakisha na akilazimisha kuondoka ndipo imuuze.
Adam Wharton
LIVERPOOL imeingia katika vita na Manchester United kwa ajili ya kuwania saini ya kiungo wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Adam Wharton, 22. Palace imeweka wazi kuwa haipo tayari kumuachia kirahisi nyota huyo na inahitaji walau Pauni 80 milioni ili kumuuza. Wharton ambaye amekuwa mchezaji tegemeo wa Crystal Palace tangu msimu uliopita, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029.
Marcos Senesi
TOTTENHAM Hotspur imefikia makubaliano ya awali ya kumsajili beki wa Bournemouth na Argentina, Marcos Senesi, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mkataba wa Senesi unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu, jambo linaloifanya Spurs itamani kumsajili kwa sababu itampata bure. Hata hivyo, dili hilo litategemea na Spurs ambayo ipo hatihati kushuka daraja, hivyo litafanyika ikiwa tu itabaki EPL.
Jeremy Monga
ARSENAL imeonyesha nia ya kumsajili winga chipukizi wa Leicester City na timu ya taifa ya England, Jeremy Monga, 16, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Monga ambaye ni mchezaji wa timu za vijana za England, anatajwa kuwa mmoja wa mastaa wenye vipaji vinavyochipukia kwa kasi. Arsenal inaendelea na mkakati wa kusajili wachezaji vijana wenye vipaji vikubwa kwa ajili ya maendeleo ya muda mrefu, na Monga anaonekana kuwa sehemu ya mkakati huo.
Yoane Wissa
NEWCASTLE United ipo tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa DR Congo, Yoane Wissa, 29, licha ya kumsajili msimu uliopita. Mabosi wa Newcastle wanataka kumuuza nyota huyo waliyemsajili Brentford kwa Pauni 50 milioni msimu uliopita ili kuendana na sheria za usawa wa matumizi. Mkataba wa sasa wa Wissa unamalizika 2028 na inadai Newcastle inaweza kuwa tayari kumuuza zaidi ya Pauni 60 milioni.
Dani Ceballos
AJAX imeonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Real Madrid na Hispania, Dani Ceballos, 29, katika dirisha lijalo majira ya kiangazi. Ceballos amekuwa hana nafasi ya uhakika katika kikosi cha Real Madrid, jambo linayoleza kumfanya kuangalia uwezekano wa kupata changamoto mpya sehemu nyingine. Ajax inataka kuongeza ubunifu katika eneo la kiungo na Ceballos anaweza kuwa nyongeza muhimu kutokana na uzoefu.
David Alaba
BEKI wa kimataifa wa Austria, David Alaba, 33, anatarajiwa kuondoka Real Madrid baada ya mkataba wake kumalizika katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Alaba amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu akitoa mchango mkubwa katika safu ya ulinzi. Kuondoka Alaba ni sehemu ya mabadiliko ya kikosi cha Real Madrid ambayo inataka kuanza upya baada ya kupitia kipindi kigumu Ulaya.
Konstantinos Mavropanos
BEKI wa kati wa West Ham United, Konstantinos Mavropanos, 28, anatarajiwa kuondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Borussia Dortmund ndio inadaiwa kuwa imeonyesha nia ya kumsajili nyota huyo wa Ugiriki, lakini ina wasiwasi kuhusu gharama ya usajili ya mchezaji huyo. Kwa sasa mazungumzo yanaendelea na ripoti zinadai Mavropanos anatamani sana kuondoka kwenda Dortmund ili kupata changamoto mpya.