Broos: Hata Salah ameishangaa ile penalti
Muktasari:
- Kwa sasa Afrika Kusini inahitaji sare yoyote dhidi ya Zimbabwe kesho Jumatatu ili kukata tiketi ya kwenda hatua ya 16 bora, lakini inaweza kukutana na njia ngumu zaidi katika hatua ya mtoano iwapo inataka kufanya vizuri zaidi ya medali ya shaba iliyoipata miaka miwili iliyopita.
BAFANA Bafana ilipata kipigo cha kuumiza juzi jioni kutoka kwa Misri iliyokuwa na wachezaji 10 katika mechi ya Kundi B ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, lakini kocha amefichua alichozungumza na mfungaji wa bao hilo pekee la penalti kwa Mafarao, Mohammed Salah.
Kwa sasa Afrika Kusini inahitaji sare yoyote dhidi ya Zimbabwe kesho Jumatatu ili kukata tiketi ya kwenda hatua ya 16 bora, lakini inaweza kukutana na njia ngumu zaidi katika hatua ya mtoano iwapo inataka kufanya vizuri zaidi ya medali ya shaba iliyoipata miaka miwili iliyopita.
Jana ilikuwa jioni ngumu hasa kutokana na uamuzi wa refa aliyetoa penalti kwa Misri kipindi cha kwanza baada ya mkono wa Khuliso Mudau kumgusa usoni Salah walipokuwa wakigombea mpira ndani ya eneo la hatari.
Baadaye, Bafana Bafana ilinyimwa penalti mwishoni mwa mechi licha ya tukio kuonekana mpira uliguswa na mkono ndani ya boksi. Hata hivyo, kilichoigharimu zaidi Bafana Bafana ni kushindwa kutumia nafasi ilizopata jambo lililoifanya iondoke bila pointi.
Haya hapa ni maoni ya kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Hugo Broos na nahodha Ronwen Williams, Mudau na kiungo Thalente Mbatha kutoka eneo la mahojiano kupitia SABC Sport.
HUGO BROOS
“Hata Salah mwenyewe aliniambia baada ya mechi kuwa alishangazwa na penalti ile. Ilikuwa ya ajabu kabisa. Katika mkutano wa kabla ya mashindano wamesema kama mkono umeachwa mbali na mwili, basi ni penalti.
"Kisha wanasema ulikuwa mkono wa kujitegemeza. Nani aliyevumbua mkono wa kujitegemeza? Mkono wake ulikuwa umeachwa wazi na mpira ukagonga mkono.
"Nataka kuzungumzia mikutano ya kabla ya mashindano. Hakuna anayejua afanye nini. Kwa dakika 45 wanaelezea sheria, kuna sheria 25 hadi 50. Leo ni penalti, kesho si penalti.
Ni kadi nyekundu leo, kesho si kadi nyekundu. Mwishowe kuna sheria nyingi kiasi kwamba hakuna anayejua cha kufanya.”
RONWEN WILLIAMS
“Tumesikitishwa. Lengo letu halikuwa kupoteza. Tulitaka kushinda au angalau kupata pointi ili kujihakikishia kufuzu, lakini haikuwezekana.
"Tunahisi tumeonewa kidogo na maamuzi ya waamuzi. Ilikuwa penalti nyepesi sana kwao na ukiangalia kilichotokea upande wetu mwishoni, tulistahili penalti. Lakini hiyo ndiyo soka. Tunajifunza, tunachukua mambo mazuri na kuendelea kuamini timu hii.
"Tulijua wangekaa nyuma kwa sababu walikuwa pungufu ya mchezaji mmoja. Walikuwa wanajilinda tu. Tulitengeneza nafasi kadhaa, lakini hatukufunga. Tulijua hawatatuacha nafasi nyuma na hilo ndilo tunalolitafuta. Kuna mafunzo mengi ya kujifunza na tutakua.
"Uchezaji ulikuwa mzuri sana. Walikuja na mfumo tofauti, hatukutarajia safu ya mabeki watano. Dakika 10 za mwanzo zilikuwa za kuzoea. Mapambano na kutokata tamaa vilikuwepo. Tulitoa kila kitu uwanjani, lakini hatukufunga. Ninajivunia vijana hawa. Tumeonyesha tunaweza kushindana na bora kabisa. Sasa tunaangalia mchezo wa Jumatatu. Tutafuzu kwa hakika.”
KHULISO MUDAU
“Sidhani kama ilikuwa penalti kwa Misri. Mwamuzi aliitoa na hatuwezi kufanya chochote. Hatukuwa na bahati. Tulijitahidi kufunga lakini haikuwezekana. Tunapaswa kuangalia mchezo unaofuata.
"Kuna mambo mazuri ya kujifunza. Kila mtu alikuwa tayari kusaidia timu. Tulikosa nafasi nyingi. Tukizitumia vizuri, tutaimarika kama timu.”
THALENTE MBATHA
“Tulitafuta ushindi kipindi cha pili, tulijaribu kushambulia zaidi. Kocha alijaribu kila kitu, lakini haikuwa siku yetu.
Inakatisha tamaa kwa sababu tuliamini ilikuwa faulo au penalti kwetu. Mwamuzi aliangalia VAR, lakini hatuwezi kusema mengi. Mwamuzi ndiye mwenye kauli ya mwisho.
"Lazima turudi kwa nguvu na tushinde Jumatatu. Ni suala la kujiamini na kuamini uwezo wetu. Tuna ubora, lakini tunapaswa kuwa makini zaidi.”