Kikosi bora hatua ya makundi, Halaand, Dembele nje
Muktasari:
- Kuchagua kikosi bora cha hatua ya makundi hakikuwa kazi rahisi, kwani wachezaji wengi waliostahili nafasi walikosa kuingia kwenye orodha hii, akiwemo Erling Haaland.
DALLAS, MAREKANI: BAADA ya michezo 72 kuchezwa, sasa tunafahamu rasmi timu 32 zilizofuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia 2026.
Lakini kabla ya kuelekeza macho kwenye hatua ya mtoano, ni vyema kutazama nyuma hatua ya makundi ambayo ilikuwa na kila kitu: kufukuzwa kwa makocha, mabao ya kuvutia, matokeo ya kushangaza na mastaa wakubwa kuonyesha uwezo wao.
Kuchagua kikosi bora cha hatua ya makundi hakikuwa kazi rahisi, kwani wachezaji wengi waliostahili nafasi walikosa kuingia kwenye orodha hii, akiwemo Erling Haaland.
Kwa kuzingatia kanuni ya kuchagua mchezaji mmoja tu kutoka kila taifa, hiki ndicho kikosi bora cha hatua ya makundi cha Kombe la Dunia 2026 kilichochaguliwa na Daily Mail Sport.
Mfumo: 4-3-3
Kipa: Vozinha (Cape Verde)
Bila shaka ndiye hadithi ya kufurahisha zaidi ya mashindano hadi sasa.
Kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 wa Cape Verde hakutarajia kabisa kuwa sehemu ya mjadala wa makipa bora kabla ya mchezo wa kwanza dhidi ya Hispania.
Baada ya kuzuia mashambulizi yote ya Hispania na kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii, Vozinha amemaliza hatua ya makundi akiwa na mechi mbili bila kuruhusu bao na amekuwa sababu kubwa ya Cape Verde kufuzu hatua ya 32 bora.
Ingawa mechi dhidi ya Saudi Arabia haikupata umaarufu kama ile ya Hispania, ilimwezesha kuingia kwenye orodha ya kipekee ya makipa waliowahi kuweka clean sheet mbili au zaidi katika Kombe la Dunia wakiwa na zaidi ya miaka 40.
Sasa ameungana na Peter Shilton (mechi tatu) na Dino Zoff (mechi mbili).
Beki wa kulia: Daniel Munoz (Colombia)
Licha ya kuanzia benchi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Ureno, Daniel Munoz alionyesha kiwango bora katika michezo miwili ya kwanza.
Nyota huyo wa Crystal Palace alikuwa mchezaji muhimu zaidi wa Colombia, akifunga mabao muhimu yaliyowahakikishia kufuzu kabla ya mchezo wa mwisho.
Dhidi ya DR Congo, nguvu zake na uwezo wa kushambulia vilifanya tofauti, huku shuti lake lililobadili mwelekeo likiwa bao la ushindi.
Pia alikaribia kuisaidia Colombia kushinda dhidi ya Ureno, jambo lililofanya wengi kushangazwa kwa nini hakuanza mchezo huo.
Pongezi pia zinamwendea Denzel Dumfries, ambaye alikuwa mgombea mkubwa wa nafasi hii.
Beki wa kati: Virgil van Dijk (Uholanzi)
Katika kundi gumu sana, Uholanzi ilimaliza bila kupoteza dhidi ya Japan, Sweden na Tunisia.
Ingawa safu yao ya ulinzi haikuwa kamilifu, Van Dijk pamoja na Jan Paul van Hecke walikuwa imara sana.
Nahodha huyo wa Liverpool amepewa nafasi hii kutokana na uongozi wake mkubwa uliowasaidia Waholanzi kutulia katika nyakati ngumu za michezo.
Mbali na hilo, alichangia bao moja na asisti moja akiwa beki wa kati.
Beki wa kati: Pau Cubarsi (Hispania)
Alicheza kila dakika katika michezo yote mitatu huku Hispania ikimaliza hatua ya makundi bila kuruhusu hata bao moja.
Katika michezo hiyo yote waliruhusu mashuti matatu tu yaliyolenga lango.
Licha ya kiwango cha wapinzani, Cubarsi ameonyesha uwezo mkubwa wa kuchezesha mpira kutoka nyuma.
Kati ya pasi 294 alizopiga, alikosea tano pekee.
Mwenza wake Aymeric Laporte pia alistahili kutajwa, lakini ubora wa Cubarsi katika kujenga mashambulizi ulimpa nafasi hii.
Ni nyota anayekuja kwa kasi.
Beki wa kushoto: Antonee Robinson (Marekani)
Marekani imeonyesha soka la kuvutia katika hatua ya makundi na ilistahili kuwa na mwakilishi katika kikosi hiki.
Ingawa takwimu zake hazionekani za kipekee, Robinson amekuwa tishio kubwa kwa mfumo wa kocha Mauricio Pochettino.
Kama ilivyo kwa Fulham, ameendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia na kurudi kusaidia ulinzi.
Kwa aina ya mfumo anaoutumia Pochettino, Robinson ni beki wa kushoto anayefaa kabisa.
Kiungo: Jude Bellingham (England)
Amekuwa mchezaji bora wa England katika michezo yote mitatu na ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi mara mbili.
England imekuwa ikikosa ubunifu mara nyingi, lakini kiwango cha Bellingham kimekuwa faraja kubwa kwa kocha Thomas Tuchel.
Alibadilisha mchezo dhidi ya Croatia na pia alifunga bao pamoja na kutoa asisti dhidi ya Panama.
Ni vigumu kuamini kwamba kabla ya mashindano kulikuwa na mjadala kama alistahili kuanza kwenye kikosi.
Kiungo: Johan Manzambi (Uswisi)
Uswisi ilikuwa katika wakati mgumu baada ya sare dhidi ya Qatar na pia ilipata shida dhidi ya Bosnia na Herzegovina.
Lakini Manzambi alipoingia kutoka benchi, kila kitu kilibadilika.
Kijana huyo mwenye miaka 20 alifunga mabao mawili dhidi ya Bosnia na baadaye akafunga bao la ushindi pamoja na kutoa asisti dhidi ya Canada.
Amejitangaza rasmi kama mmoja wa nyota wanaochipukia katika Kombe hili la Dunia.
Kiungo: Ismael Saibari (Morocco)
Kiungo huyo anayetarajiwa kujiunga na Bayern Munich amefunga katika kila mchezo wa hatua ya makundi na kuiongoza Morocco hadi hatua inayofuata.
Kwa kufunga dhidi ya Haiti, Saibari aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kufunga katika kila mchezo wa hatua ya makundi wa Kombe la Dunia.
Pia amekuwa Mwafrika wa kwanza kufunga mabao matatu katika Kombe la Dunia tangu Asamoah Gyan mwaka 2010.
Winga wa kulia: Lionel Messi (Argentina)
Mchezaji bora zaidi kuwahi kucheza mchezo huu.
Alianza mashindano kwa hat-trick dhidi ya Algeria, kisha akaongeza mabao mawili dhidi ya Austria.
Argentina ilipofuzu mapema, alianza mchezo wa mwisho akiwa benchi.
Akiwa na miaka 39 bado anaonekana mwenye nguvu na ubora mkubwa.
Amefunga mabao matano na kwa sasa anaongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu.
Mshambuliaji: Kylian Mbappe (Ufaransa)
Licha ya ubora wa Messi, Mbappe ameonyesha kuwa Kombe hili linaweza kuwa lake.
Anaongoza kwa jumla ya mabao na asisti kuliko mchezaji mwingine yeyote katika mashindano.
Alifunga mabao mawili dhidi ya Senegal na Iraq, huku pia akitoa asisti mbili kwa Ousmane Dembele dhidi ya Norway.
Kwa kasi, nguvu ya mashuti na kujiamini kwake, ndiye mchezaji anayewaogopesha zaidi wapinzani katika hatua ya mtoano.
Winga wa kushoto: Vinicius Junior (Brazil)
Brazil bado inaonekana haijaonyesha uwezo wake wote, lakini Vinicius tayari ameanza kung'ara.
Alifunga bao muhimu la kusawazisha dhidi ya Morocco, akachangia bao na asisti dhidi ya Haiti, kisha akafunga mabao mawili dhidi ya Scotland.
Kwa ujumla amehusika katika asilimia 71 ya mabao yote ya Brazil katika Kombe hili la Dunia.
Neymar amesema:"Vinicius Jr ndiye nyota wetu katika Kombe hili la Dunia. Anaamua michezo na anafanya vizuri sana."
Kwa uwezo wake mkubwa na kujiamini, Vinicius ni aina ya mchezaji aliyezaliwa kwa ajili ya kuangaza katika hatua za mtoano za Kombe la Dunia.