Kishindo cha Mourinho El Clásico
Muktasari:
- Mourinho alisherehekea ushindi huo kwa mtindo wake wa kipekee wa kuteleza kwa magoti uwanjani, baada ya Kylian Mbappe kufunga bao la ushindi lililoihakikishia Real Madrid pointi tatu muhimu katika Uwanja wa Camp Nou.
BARCELONA, HISPANIA: KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho, ameendelea kuonyesha makali yake katika pambano la watani wa jadi, El Clásico, baada ya kuiongoza timu hiyo kuichapa Barcelona mabao 2-1 katika mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, Jumapili.
Mourinho alisherehekea ushindi huo kwa mtindo wake wa kipekee wa kuteleza kwa magoti uwanjani, baada ya Kylian Mbappe kufunga bao la ushindi lililoihakikishia Real Madrid pointi tatu muhimu katika Uwanja wa Camp Nou.
Ushindi huo umeendeleza rekodi nzuri ya Mourinho dhidi ya Barcelona, akifikisha mechi sita mfululizo za El Clásico bila kupoteza, ikiwa ni miaka 13 tangu alipokuwa akiiongoza Real Madrid katika pambano hilo.
Katika mechi zake sita zilizopita za El Clásico akiwa benchi la Real Madrid, Mourinho amepata ushindi mara nne na sare mbili, rekodi inayomweka katika kundi la makocha wachache wa Los Blancos waliowahi kufanya hivyo.
Makocha wengine waliofikia mafanikio hayo ni Miguel Muñoz, aliyefanya hivyo kati ya mwaka 1962 na 1965, pamoja na Vicente del Bosque, aliyefanikiwa kati ya mwaka 2001 na 2003.
Matokeo ya Jumapili yamekuwa pigo kubwa kwa Barcelona, ambayo ilikuwa imecheza mechi tisa mfululizo bila kupoteza katika mashindano ya ndani ya Hispania.
Mbappe alikuwa shujaa wa Real Madrid baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi huo wa mabao 2-1, uliovunja rekodi ya kutopoteza ya Barcelona na kuipa Real Madrid nafasi muhimu katika mbio za ubingwa wa La Liga.
Kabla ya mchezo huo, Real Madrid ilikuwa na presha kubwa, kwani kushindwa kungeipa Barcelona nafasi ya kujitanua kwa tofauti ya pointi tisa kileleni mwa msimamo wa ligi.
Hata hivyo, ushindi huo umebadili hali ya mbio za ubingwa, huku Real Madrid ikiipunguzia Barcelona tofauti ya pointi hadi tatu na kuifanya La Liga kuendelea kuwa na ushindani mkali.
Akizungumza baada ya mchezo, Mourinho amesema lengo la Real Madrid si kupata ushindi dhidi ya Barcelona pekee, bali kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kutwaa ubingwa wa ligi.
“Kwa mtazamo wangu, Real Madrid haiendi Camp Nou kucheza ili kushinda tu dhidi ya Barcelona, bali inaenda kushinda La Liga,” amesema Mourinho.
Aliongeza kuwa ushindi huo haukutokana na bahati, bali utulivu na ubora wa wachezaji wake uwanjani.
“Tungeweza kushinda kwa bahati, lakini tulishinda kwa utulivu na kwa haki kabisa. Hili ni kundi imara sana. Kila mmoja anafanya kazi kwa bidii na wote walikuwa tayari kushinda,” amesema.
Licha ya furaha ya ushindi huo mkubwa, Mourinho alikataa kujipa sifa binafsi, akisisitiza kuwa mafanikio ya Real Madrid yanatokana na mchango wa wachezaji wake.
Kocha huyo raia wa Ureno amesema mara nyingi makocha wamekuwa wakilaumiwa na kufukuzwa kazi timu zinapofanya vibaya, lakini sifa za ushindi zinapaswa kwenda kwa wachezaji.
“Sifa zinastahili wachezaji. Unaposhinda, sifa huenda kwa wachezaji, lakini unapopoteza lawama zinakuangukia wewe. Ndiyo maana tunaona makocha wakifukuzwa kazi kila wiki,” amesema.
Mourinho, ambaye kwa sasa ana rekodi ya kushinda mechi sita na kupoteza sita katika jumla ya mechi za El Clásico katika vipindi vyake viwili vya kuifundisha Real Madrid, amesema mchezo huo umempa picha halisi ya uwezo wa kikosi chake.
“Nimejifunza kuwa nina kikosi cha kipekee, chenye ubora na mtazamo sahihi wa kucheza,” amesema.
Alieleza kuwa mchanganyiko wa vipaji tofauti katika safu ya kiungo umeipa timu yake uwiano mzuri wa kukaba na kushambulia.
“Tunapokuwa na mchanganyiko wa vipaji katikati ya uwanja, tunapata zaidi kuliko kuwa na wachezaji wawili wenye sifa zinazofanana. Mchanganyiko huo unatupa uwiano mzuri tunapokaba na ubora tunapoenda kushambulia,” amesema.
Mourinho alisisitiza kuwa ingawa Real Madrid imewahi kuzifunga timu kadhaa kwa tofauti ya mabao manne au zaidi, ushindi dhidi ya Barcelona una uzito wa kipekee.
“Hii ni Barcelona, na wachezaji walifanya kazi kubwa. Tunapaswa kuendelea hivi na tusijisahau kutokana na ushindi huu,” ameonya.