Manchester yatua West Ham ikimtaka Mateus
Muktasari:
- Inadaiwa kwamba Manchester United wameulizia uwezekano wa kumsajili kiungo huyo walipojihakikishia kwamba timu yake haitatoboa juzi usiku, lakini wanatarajiwa kukumbana na upinzani mkali kutoka wka Arsenal na Paris Saint-Germain ambazo pia zinamfuatilia mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 21, anayekadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 80 milioni.
MARA tu baada ya kuthibitika kwamba timu yake imeshuka daraja, Manchester United imetua West Ham United ikimuwinda kiungo Mateus Fernandes katika dili ambalo huenda likakamilika mapema zaidi kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2026 hazijaanza mwezi ujao.
Inadaiwa kwamba Manchester United wameulizia uwezekano wa kumsajili kiungo huyo walipojihakikishia kwamba timu yake haitatoboa juzi usiku, lakini wanatarajiwa kukumbana na upinzani mkali kutoka wka Arsenal na Paris Saint-Germain ambazo pia zinamfuatilia mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno mwenye umri wa miaka 21, anayekadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 80 milioni.
Inaelezwa kwa sasa Mashetani Wekundu wanakamilisha taratibu za kuwasilisha ofa rasmi kwa West Ham United na mchezaji husika ili kuanzisha mazungumzo ambayo huenda yakashuhudia wakiondoka na nyota huyo kabla mwezi ujao haujaanza.
Kwa upande wa Arsenal na PSG, inadaiwa zimeonyesha nia ya kumtaka, lakini hadi jana zilikuwa haziwasiliana na kambi yake wala uongozi wa timu inayommiliki. Kushuka kwa West Ham United kunatarajiwa kushuhudia mastaa kibao wakiondoka katika dirisha lijalo la usajili mara tu litakapofunguliwa.
EDERSON
SUPASTAA wa Atalanta na Brazil, Ederson Jose dos Santos Lourenco da Silva maarufu Ederson anadaiwa kuwa katikati ya mazungumzo na
Manchester United ikielezwa kwamba yapo hatua za juu na pia Atalanta ikihusishwa kwa ukaribu.
Mchezaji huyo wa kiungo mwenye umri wa miaka 26, ingawa bado kuna tofauti ya thamani ya mchezaji huyo kati ya klabu hizo mbili, lakini kuna kila dalili kwamba mambo huenda yakamalizika haraka ili kurahisisha ratiba mbalimbali zinazokikabili kikosi hicho katika siku za usoni. Ederson anatarajiwa kumaliza mkataba Atalanta Juni 30, mwakani.
PAULO DYBALA
SAA chache baada ya kujihakikishia kubaki Ligi Kuu England, Tottenham Hotspur imeongeza spidi kufukuzia saini ya mshambuliaji wa AS Roma, Paulo Dybala, 32, ili kwenda kuongeza nguvu katika kikosi hicho cha jijini London ambacho kinatarajiwa kusukwa upya na Kocha Roberto De Zerbi kwa ajili ya msimu ujao.
Kinachofahamika ni kwamba, De Zerbi anatarajia kuachana na baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakishutumiwa kutojituma ipasavyo kikosini ikizingatiwa wana majina na uwezo mkubwa uwanjani.
Dybala amekuwa akisotea namba katika kikosi cha Roma na mkataba wake unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 30, mwaka huu.
ROMEO LAVIA
BAADA ya kukosa nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, Chelsea iko tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya wachezaji kadhaa wakiwamo Romeo Lavia, Wesley Fofana, Andrey Santos, Pedro Neto na Malo Gusto kuanzia mwezi ujao katika kile kinachoelezwa kwamba ni 'safisha safisha' inayokuja Stanford Bridge.
Hata hivyo, mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu England na Ulaya wanaweza kukumbana na wakati mgumu kuachana na baadhi ya wachezaji kutokana na kuwa na mikataba ya muda mrefu na hivyo ili kumalizana nao zitahitajika fedha nyingi ama kuvunja mikataba au kuendelea kuwalipa sehemu ya mishahara wakitumikia timu zingine kwa mkopo.
COLE PALMER
WINGA wa Chelsea, Cole Palmer anaweza kuvutiwa kuondoka Chelsea na huenda akapenda kuungana tena na kocha wake wa zamani, Enzo Maresca katika kikosi cha Manchester City au kusikilizia ofa ya Manchester United ambayo amekuwa akihusishwa nayo kwa muda mrefu.
Palmer, 24, ni miongoni mwa wachezaji ambao mabosi wa Chelsea wamekuwa wakitamani kutosikiliza ofa ikitua mezani kwao, kwani wanaamini katika uwezo na mbinu zake kwamba zina msaada mkubwa kwa maendeleo ya baadaye ya timu yao.
Nyota huyo aliyeachwa kikosini England kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2026 anamaliza mkataba Chelsea 2033.
LEWIS HALL
BEKI wa kushoto wa Newcastle United, Lewis Hall, 21, anafikiria kuondoka baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha England cha Kombe la Dunia, huku Manchester United ikiwa miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa muda mrefu na zimehamasishwa na kutotaka kwake kurejea London.
Hall amekuwa akitamani kuondoka Newcastle tangu dirisha lililopita, na lile la Januari mwaka huu alibakiza hatua chache kutimkia Sunderland ambayo ilionyesha kutamani saini yake. Mchezaji huyo ana mkataba na Newcastle United hadi Juni 30, 2029.
ALISSON BECKER
LICHA ya kusita mwanzoni, Liverpool sasa wako tayari kumuuza kipa Alisson Becker baada ya mazungumzo na nyota huyo wa kimataifa wa Brazil, ambapo wanahitaji takriban Pauni 15 milioni, huku wababe wa Ligi Kuu Italia (Serie A), Juventus wakitajwa.
Hata hivyo, uwezekano wa kuondoka kwake utategemea timu itakayofikia kiwango hicho cha fedha kilichopo katika mkataba wake unaomalizika 2027 ili kuuvunja.
Katika siku za karibuni Becker amekuwa akilaumiwa na mashabiki wa Liverpool kutokana na ubora wake kupungua.
FRANCO MASTANTUONO
REAL Madrid wako tayari kumtoa kwa mkopo winga wa kimataifa wa Argentina, Franco Mastantuono, 18, msimu ujao baada ya kukosa namba ya kuanza katika kikosi cha wababe hao wa Ligi Kuu Hispania (LaLiga).
Hata hivyo, katikati ya mpango huo inaelezwa kwamba Tottenham Hotspur ambayo imethibitisha kubaki Ligi Kuu England inaonekana kuanza kufukuzia saini yake na lolote linaweza kutokea kati ya sasa na mwezi ujao.
Mastantuono amewahi kukaririwa akiomba kuondoka Real Madrid ili kwenda kukuza kipaji katika timu zingine kwenye ligi za Ulaya ambako timu mbalimbali zimewahi kuonyesha nia ya kuwa naye.