Marcus Rashford apendekezwa Real Madrid
Muktasari:
- Kwa mujibu wa gazeti la Sport la Hispania, Mourinho anaamini Rashford mwenye umri wa miaka 28 anaweza kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Real Madrid iwapo atarejea kuinoa klabu hiyo.
KOCHA mbwatukaji anayehusishwa na Real Madrid, Jose Mourinho anaripotiwa kupendekeza majina ya washambuliaji kadhaa anaotaka wasajiliwe ikiwa atajiunga na klabu hiyo na miongoni mwao ni mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Barcelona.
Kwa mujibu wa gazeti la Sport la Hispania, Mourinho anaamini Rashford mwenye umri wa miaka 28 anaweza kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Real Madrid iwapo atarejea kuinoa klabu hiyo.
Ripoti hizo zinaeleza mustakabali wa Rashford bado haujawekwa wazi kwa sababu Barcelona bado inasita kulipa Euro 30 milioni zinazohitajika na Man United ili kumnunua fundi huyo mazima.
Hali hiyo imefungua mlango kwa klabu nyingine ikiwemo Aston Villa ambayo ipo tayari kulipa zaidi ya hiyo Euro 30 milioni ambayo Barcelona inapata wakati mgumu kuilipa.
Hata hivyo, Rashford mwenyewe macho na masikio yake yote yapo Barca akiweka wazi kuwa ndiyo timu pekee anayoipa kipaumbele cha kujiunga nayo kwa dirisha lijalo.
Rashford amekuwa akimezewa mate na vigogo mbalimbali Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha msimu huu akiwa na Barca ambapo amefunga maba 14 katika mechi 48 za michuano yote.
William Osula
EVERTON pamoja na Aston Villa zinadaiwa kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Newcastle United na Denmark, William Osula, katika dirisha lijalo.
Taarifa za uhakika zinadai klabu hizo mbili za Ligi Kuu England zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya mshambuliaji huyo, 22, ambaye hakupata nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha Newcastle kwa msimu uliopita.
Mkataba wa sasa wa Osula unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 na msimu huu amecheza mechi 34 za michuano yote na kufunga mabao tisa.
Levi Colwill
CHELSEA bado haijaanza mazungumzo rasmi ya kumpatia beki wao wa kati raia wa England, Levi Colwill, mkataba mpya wenye masilahi yaliyoboreshwa.
Ingawa hakuna mazungumzo yanayoendelea kwa sasa, kuna uwezekano mkubwa wa pande zote kurejea mezani dirisha lijalo.
Colwill, 23, ameendelea kuwa sehemu muhimu ya beki ya Chelsea kutokana na kiwango bora anachoonyesha mara zote anapopewa nafasi ya kucheza. Ripoti zinaeleza Chelsea bado wanaamini beki huyo ni sehemu ya mipango yao ya muda mrefu.
Karim Adeyemi
MANCHESTER United na Chelsea bado zipo vitani kuiwania saini ya mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi, dirisha lijalo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Teamtalk, Dortmund ipo tayari kumuuza nyota huyo, 24, iwapo itapata ofa inayoridhisha.
Adeyemi ameendelea kuvutia macho ya klabu kubwa Ulaya kutokana na kasi yake, uwezo wa kucheza nafasi tofauti za ushambuliaji pamoja na uzoefu wake katika michuano ya Ulaya.
Mkataba wake unamalizika mwakani na msimu huu amecheza mechi 39 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Lutsharel Geertruida
BEKI wa kati wa RB Leipzig, Lutsharel Geertruida ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Sunderland, inadaiwa ana nia ya kuendelea kusalia katika klabu hiyo na kucheza EPL msimu ujao.
Mchezaji huyo, 25, alionyesha kiwango bora Sunderland kiasi cha mabosi wa klabu hiyo kuanza mchakato wa kumsainisha mkataba wa moja kwa moja.
Everton pia ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa karibu fundi huyu na huenda ikaipiku Sunderland.
Antonio Rudiger
REAL Madrid inadaiwa kufikia makubaliano na beki wao kisiki kutoka Ujerumani, Antonio Rudiger, ambaye atasaini mwaka mmoja ili kuendelea kubakia Santiago Bernabéu.
Inaelezwa Rudiger, 33, alikuwa akifikiria kuondoka mwisho wa msimu huu, hususani baada ya klabu kadhaa za England ikiwemo Chelsea kuonyesha nia ya kutaka kumsajili tena.
Hata hivyo, mbali yakuwa imefikia makubaliano ya kumsainisha mkataba mpya beki huyo, inaelezwa Madrid inafikiria kuwasilisha ofa kwenda Manchester City ili kumsajili beki wa klabu hiyo, Josko Gvardiol.
Tom Heaton
MANCHESTER United wanaripotiwa kuwa karibu kumpa mkataba mpya wa mwaka mmoja kipa mkongwe wa kimataifa wa England, Tom Heaton, ambao utamruhusu kuendelea kubaki Old Trafford kwa msimu wa sita.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Mirror, uamuzi huo umefanywa na Kocha Michael Carrick ambaye anamwona staa huyo kama kiongozi mbali ya uzoefu wake wa katika lango.
Heaton amekuwa sehemu ya kikosi cha Man United kwa muda mrefu akiwa anatumika kama kipa namba mbili.
Denzel Dumfries
LIVERPOOL inaripotiwa kuwa katika mipango ya kumsajili beki wa kulia wa kimataifa wa Uholanzi, Denzel Dumfries ili kuimarisha safu yao ya beki msimu ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya Football Insider, Dumfries, 30, anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuondoka Inter ikiwa ofa nzuri itawasilishwa dirisha lijalo.
Liverpool inaamini moja kati ya maeneo ambayo yamewafelisha sana msimu huu ni beki wa kulia. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.