Rufaa ya Senegal kupinga kuvuliwa ubingwa AFCON kusikilizwa Oktoba 8
Muktasari:
- Kikao hicho kitafanyika kwa faragha mjini Lausanne, Uswisi, na kinatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu sakata hilo lililozua mjadala mkubwa.
MAHAKAMA ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), imetangaza kwamba, Oktoba 8, 2026, itasikiliza rufaa ya Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) dhidi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF), kufuatia Senegal kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Kikao hicho kitafanyika kwa faragha mjini Lausanne, Uswisi, na kinatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu sakata hilo lililozua mjadala mkubwa.
CAS ndiyo chombo cha juu zaidi cha kisheria katika michezo kitakachoamua iwapo Senegal, ambayo ilishinda fainali ya AFCON 2025 uwanjani au Morocco, ambayo baadaye ilikabidhiwa taji hilo, ndiyo itatambuliwa rasmi kuwa bingwa wa mashindano hayo.
Katika taarifa iliyotolewa Julai 24, 2026, CAS ilisema: "Rufaa ya FSF inalenga kubatilisha uamuzi wa CAF uliotangaza kuwa timu ya taifa ya Senegal ilipoteza fainali ya AFCON 2025 kwa kujitoa, na kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0. Rufaa hiyo pia inaiomba CAS kuitangaza Senegal kuwa bingwa halali wa AFCON 2025."
CAS ilieleza kuwa pande zote zinazohusika hazikukubaliana kuharakisha mchakato wa kesi hiyo, hivyo itafuata ratiba ya kawaida kwa mujibu wa kanuni za mahakama hiyo.
"Tarehe ya usikilizwaji wa kesi imepangwa baada ya mashauriano na pande zote, ambazo pia hazikuomba kikao hicho kiwe wazi kwa umma. Hivyo, usikilizwaji utafanyika kwa faragha."
Mahakama hiyo imeongeza kuwa, baada ya usikilizwaji kukamilika, jopo la majaji litaanza kujadili uamuzi wake.
"Kwa sasa CAS haiwezi kusema ni lini uamuzi wa mwisho utatolewa, lakini hautatangazwa siku ya usikilizwaji wa kesi."
Katika fainali iliyochezwa Januari 18, 2025 mjini Rabat nchini Morocco, Senegal ilitoka uwanjani kupinga uamuzi wa waamuzi baada ya kunyimwa bao la ushindi dakika za mwisho na baadaye mwamuzi wa DR Congo, Jean-Jacques Ndala, kuipa Morocco penalti.
Baada ya mchezo kusimama kwa dakika 14, ulianza tena, lakini Brahim Diaz alikosa penalti hiyo alipokuwa akijaribu kuipiga kwa mtindo wa Panenka.
Mchezo uliendelea hadi muda wa nyongeza, ambapo Pape Gueye aliifungia Senegal bao pekee lililoipa ushindi wa 1-0 na kutwaa taji la AFCON.
Hata hivyo, baada ya Kamati ya Nidhamu ya CAF awali kutoa faini pekee, Kamati ya Rufaa ya CAF baadaye ilibatilisha matokeo hayo, ikaivua Senegal ubingwa na kutangaza Morocco kuwa bingwa rasmi.
Sasa Senegal imekata rufaa CAS ikiwa na matumaini ya kurejeshewa ubingwa wa AFCON 2025.