Tottenham yaongeza nguvu kuisaka saini ya Savinho
Muktasari:
- Kabla ya mwisho wa wiki iliyopita, Spurs ilikuwa haina uhakika wa kubaki katika michuano hiyo na hivyo ilikuwa imesitisha michakato yote inayohusiana na usajili wa wachezaji wapya wala kuboresha mikataba ya nyota wake kikosini kwa sababu ilikuwa ikifikiria namna ya kuishi bila kuwa na majina makubwa iwapo ingedondokea Champuionship.
TOTTENHAM Hotspur wamefufua tena nia yao ya kumsajili winga wa Manchester City na Brazil, Savio Moreira de Oliveira maarufu Savinho, 22, katika dili linaloweza kufikia Pauni 60 milioni, baada ya timu hiyo kujihakikishia kubaki Ligi Kuu England msimu ujao.
Kabla ya mwisho wa wiki iliyopita, Spurs ilikuwa haina uhakika wa kubaki katika michuano hiyo na hivyo ilikuwa imesitisha michakato yote inayohusiana na usajili wa wachezaji wapya wala kuboresha mikataba ya nyota wake kikosini kwa sababu ilikuwa ikifikiria namna ya kuishi bila kuwa na majina makubwa iwapo ingedondokea Champuionship.
Savinho ambaye amekumbana na upinzani mkali wa kupata namba katika kikosi cha Man City, katika siku za karibuni pia anakabiliwa na majeraha ya mara kwa mara. Hata hivyo kuondoka kwa Kocha Pep Guardiola kunaweza kumfanya kuanza kufikiria upya uamuzi wake wa kuondoka City na hivyo huenda hata Spurs ikajikuta ikishindwa kumng'oa. Mkataba wa nyota huyo unamalizika 2031.
YAN DIOMANDE
LIVERPOOL imeongeza kasi katika mpango wake wa kunasa kipaumbele chake ambacho ni mbadala wa Mohamed Salah, huku winga wa RB Leipzig na Ivory Coast, Yan Diomande, 19, akiendelea kuongoza katika orodha ya nyota wanaofuatiliwa.
Diomande ana kipengele cha kuondoka RB Leipzig cha Pauni 86 milioni, ambacho kwa Liverpool iliyoongoza Ligi Kuu England kwa matumizi makubwa ya fedha za usajili msimu uliopita huenda kisiwe kikubwa sana.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England 2024/25 pia wajumuisha majina ya Anthony Gordon wa Newcastle United na Bradley Barcola anayekipiga Paris Saint-Germain kama mbadala iwapo watamkosa Diomande.
MARCUS RASHFORD
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na England, Marcus Rashford, 28, ameshamalizana na Barcelona kila kitu na kwa sasa kinachosubiriwa ni kumalizika kwa mazungumzo yaliyoanza upya ambayo timu hiyo ingependa yamalizike kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia huko Amerika Kaskazini, Juni 11, 2026.
Inadaiwa katika makubaliano binafsi na mchezaji huyo aliyekuwa kwa mkopo Barcelona msimu uliomalizika timu hiyo imeamua kumpunguzia malipo ya mshahara wake wa sasa wa Pauni 325,000 kwa wiki ambapo atapokea zaidi kidogo ya nusu ya kiwango hicho. Rashford ana mkataba Man United hadi Juni 30, 2028.
ENZO FERNANDEZ
KIUNGO wa Chelsea na timu ya taifa ya Argentina, Enzo Fernandez, 25, ameibuka kuwa kipaumbele kikuu cha usajili wa majira ya joto kwa Manchester City, huku taarifa pia zikimhusisha na Real Madrid ambako kuna uwezekano mkubwa likapita panga katika eneo hilo kikosini.
Hata hivyo, kuibuka ghafla kwa Man City kumeshangaza kwani awali haikuwahi kabisa kumzungumzia mchezaji na hivyo huenda ikawa ni mipango ya kocha mpya baada ya Pep Guardiola kuondoka hivi karibuni.
Kwa sasa kinachoelezwa ni kwamba Enzo hana mpango wa kuondoka Stamford Bridge hadi Juni 30, 2032.
MASON GREENWOOD
AS Roma wameanza kumuwania mshambuliaji wa Klabu ya Marseille na England, Mason Greenwood ambaye amekuwa katika misuguano ya hapa na pale na mashabiki wa timu yake kutokana na kushuka kwa kiwango pamoja na tabia zake za nje ya uwanja.
Hata hivyo, timu hiyo ya Italia pia inawataka nyota wengine wawili, Joshua Zirkzee wa Manchester United na winga wa West Ham United, Crysencio Summerville ikiwa ni lengo la maandalizi ya mapema kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Ukiachana na Greenwood na Summerville, Zirkzee hana namba ya uhakika kikosini Man United.
HARVEY BARNES
ASTON Villa wanafikiria kumsajili winga wa Newcastle United, Harvey Barnes, 28, wakilenga kuboresha kikosi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, ambapo wamekuwa wakipambana zaidi kuboresha eneo hilo hususan kushoto bila mafanikio.
Barnes amekuwa sehemu ya mafanikio ya Newcastle United katika misimu ya karibuni na kumekuwapo na juhudi mbalimbali za timu kubwa Ulaya kutaka kumng'oa England zikiwamo za Ligi Kuu Hispania (LaLiga).
KENNET EICHHORN
KIUNGO wa Hertha Berlin na Ujerumani, Kennet Eichhorn mwenye umri wa miaka 16 ameingia kwenye rada za Liverpool inayomtaka kwenda kumuunganisha na wachezaji wake wenye umri mdogo kwa ajili ya kuendelea kuandaa kikosi cha muda mrefu cha timu hiyo.
Mchezaji huyo amekuwa kivutio katika mashindano ya ligi ya vijana wa umri huo nchini Ujerumani, huku akivutia macho ya wasaka vipaji wa timu mbalimbali Ulaya.
Liverpool inaweza kukumbana na wakati mgumu kuinasa saini ya Eichhorn anayechukuliwa kuwa miongoni mwa nyota wajao Ulaya.
LEWIS HALL
BEKI wa kushoto wa England na Newcastle United, Lewis Hall, 21, anawezaa kuondoka, huku Manchester United ikiwa miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa muda mrefu na zimehamasishwa na kutotaka kwake kurejea London.
Hall amekuwa akitamani kuondoka Newcastle tangu dirisha lililopita, na lile la Januari mwaka huu alibakiza hatua chache kutimkia Sunderland ambayo ilionyesha kutamani saini yake. Mchezaji huyo ana mkataba na Newcastle United hadi Juni 30, 2029.