Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushindi wa Anton Joshua ‘shaka tupu’

JOSHUA Pict

Muktasari:

  • Joshua alirejea ulingoni baada ya miezi saba nje ya mchezo na kuonekana yupo ukingoni mwa kipigo katika raundi ya kwanza baada ya kudondoshwa mara mbili na bondia wa Albania, Kristian Prenga.

JEDDAH, SAUDI ARABIA: MCHAMBUZI maarufu wa michezo, Simon Jordan, ametia shaka ushindi wa Bondia Anthony Joshua dhidi ya Kristian Prenga, akidai kuna mambo "hayako sawa" kuhusu namna pambano hilo lilivyobadilika ghafla na kufungua njia ya pambano kubwa dhidi ya Tyson Fury.

Joshua alirejea ulingoni baada ya miezi saba nje ya mchezo na kuonekana yupo ukingoni mwa kipigo katika raundi ya kwanza baada ya kudondoshwa mara mbili na bondia wa Albania, Kristian Prenga.

Prenga alimwangusha Joshua kwa ngumi kali ya 'uppercut' ndani ya sekunde 20 za mwanzo wa pambano, kabla ya kumdondosha tena baadaye katika raundi hiyo. Wakati huo mashabiki wengi walihofia ndoto ya pambano la Joshua dhidi ya Tyson Fury ingeweza kufa.

JOSH 01

Hata hivyo, raundi ya pili iligeuka kabisa. Joshua alianza kushambulia kwa nguvu, akambana Prenga kwenye kamba za ulingo kabla ya kumpiga ngumi kali iliyomwangusha na kumaliza pambano kwa knockout (KO).

Ushindi huo, pamoja na Fury kumshinda Mariusz Wach siku moja kabla, umefungua rasmi njia ya pambano kubwa kati ya mabondia hao wawili wa Uingereza, ambalo linatarajiwa kuwa miongoni mwa yanayoingiza fedha nyingi zaidi katika historia ya ndondi.

JOSH 02

Jordan hakuamini kilichotokea

Kupitia mitandao ya kijamii aliandika:"Sikubaliani kabisa na pambano hilo la Anthony Joshua. Anadondoshwa mara mbili halafu ghafla ndiye anayeongoza pambano? Inawezekanaje? Prenga alikuwa tofauti kabisa raundi ya pili. Kuna jambo haliko sawa. Inaonekana kila kitu kimepangwa ili kuingiza fedha nyingi iwezekanavyo."

Takwimu za pambano zinaonyesha tofauti kubwa kati ya raundi hizo mbili. Katika raundi ya kwanza Joshua alipiga ngumi 22, lakini tano pekee zilimpata mpinzani, huku Prenga akifanikiwa kupiga ngumi 15 kati ya 32.

Raundi ya pili hali ilibadilika kabisa. Joshua alipiga ngumi 46 na 13 zikampata Prenga, wakati bondia huyo wa Albania alipiga ngumi 17 lakini tatu pekee ndizo zilizoingia.

JOSH 03

Licha ya maneno ya Jordan, Joshua alisisitiza kuwa ushindi wake umetokana na moyo wa bingwa.

"Prenga alinipa mtihani mzuri, lakini hivi ndivyo mabingwa wanavyofanya. Tunaanguka lakini tunainuka. Hivyo ndivyo maisha yalivyo," amesema Joshua.

Alimshukuru pia mpinzani wake kwa pambano zuri na kumpongeza kwa kiwango alichoonyesha.

"Ni bondia mwenye nguvu. Nafikiri Eddie Hearn sasa atataka kumsajili. Ana maisha mazuri ya baadaye kwenye ndondi."

Akizungumzia pambano linalosubiriwa dhidi ya Tyson Fury, Joshua aliwauliza mashabiki waliokuwa ukumbini:"Tyson Fury yupo humu au hayupo?"

JOSH 04

Kisha akaongeza:"Namheshimu kwa yote aliyofanya kwenye mchezo huu, lakini sasa muda wa kupigana umefika. Natumaini mashabiki watashuhudia pambano la kipekee."

Baada ya ushindi huo, Joshua alishindwa kuzuia hisia alipokumbuka marafiki zake wa karibu, Sina Ghami na Latif 'Latz' Ayodele, waliopoteza maisha katika ajali ya gari nchini Nigeria mwezi Desemba.

Joshua alipigana akiwa amechapisha majina yao kwenye kaptura zake za kijeshi, huku pia akivaa koti maalumu lenye majina yao wakati akiingia ulingoni.

Alipoulizwa jinsi alivyoweza kupitia kipindi hicho kigumu, Joshua amesema kwa sauti ya huzuni:

"Imekuwa ngumu sana... hao walikuwa ndugu zangu. Sitaki kuzungumzia hilo."

JOSH 05

Kwa upande wake, promota wake Eddie Hearn alikiri kuwa alihofia Joshua alirejea ulingoni mapema mno.

"Hakuna anayejua alipitia nini katika miezi saba iliyopita. Alipoanguka raundi ya kwanza nilihisi huenda tumemrudisha mapema sana. Lakini ndondi ndizo zimempa nguvu ya kuendelea. Kilichotokea usiku huu ni cha ajabu," amesema Hearn.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwenye pambano la Joshua dhidi ya Fury, ambalo mikataba yake tayari imesainiwa, huku tarehe na ukumbi vikisubiri kuthibitishwa rasmi.