Vita ya Julian Alvarez, Barcelona yapigwa presha na Arsenal, PSG
Muktasari:
- Álvarez ambaye kwa sasa ndiye mshambuliaji tegemeo wa Atletico mara kadhaa mwaka jana aliripotiwa yupo tayari kurudi England kujiunga na Arsenal.
BARCELONA bado inaendelea kusukuma kwa nguvu dili la kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Argentina, Julian Alvarez mwenye umri wa miaka 26.
Hata hivyo, inakumbana na ushindani mkali kutoka kwa Arsenal na Paris Saint-Germain ambazo zinatamani sana huduma ya fundi huyu wa zamani wa Manchester City.
Álvarez ambaye kwa sasa ndiye mshambuliaji tegemeo wa Atletico mara kadhaa mwaka jana aliripotiwa yupo tayari kurudi England kujiunga na Arsenal.
Kwa sasa hakuna mazungumzo rasmi yaliyoanza baina ya Barca na viongozi wa Atletico, ingawa vyombo vya habari kutoka Hispania vinadai Barca inafanya majadiliano na wakala wa staa huyo.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa Barca inaonekana kwenye kulipa ada ya uhamisho ya Alvarez ambayo inaweza kufikia Euro 80 milioni.
Changamoto hiyo inawaweka katika hatari ya kumkosa Alvarez kwani klabu nyingine zinazomhitaji PSG na Arsenal zinaweza kulipa kiasi hicho cha pesa bila wasiwasi wowote.
Rafael Leao
MANCHESTER United inaweza kumgeukia winga wa AC Milan na Ureno, Rafael Leao, 26, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ripoti zinaeleza Milan ipo tayari kumwachia fundi huyo na inaweza kuhitaji kufanya mabadilishano ya wachezaji akiwamo Marcus Rashford, 28, Manuel Ugarte, 25, au Joshua Zirkzee, 24.
Leao ni mmoja wa wachezaji tegemeo katika Milan kwa sasa na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Elliot Anderson
MANCHESTER United haina nia ya kuingia vitani kwa ajili ya kiungo wa Nottingham Forest na England, Elliot Anderson, 23, ambaye anawindwa na Manchester City.
Kutokana na uwepo wa timu nyingi zinazomhitaji, mashetani hao wekundu wanadaiwa kuelekeza nguvu zao kwa kiungo wa kimataifa wa Cameroon anayeichezea Brighton , Carlos Baleba, 22.
Baleba anatajwa kuwa chaguo la kuvutia kwa benchi la ufundi la Man United ingawa changamoto kubwa inaonekana ni bei yake inayodaiwa kufikia Pauni 70 milioni.
James Trafford
NEWCASTLE United inapanga kufanya mabadiliko makubwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi, huku nafasi ya kipa namba moja ikiwa ni miongoni mwa maeneo wanayotaka kuyaimarisha.
Majina yanayotajwa kuwa katika rada zao kwa sasa ni kipa wa Lens ya Ufaransa, Robin Risser, 21, pamoja na kipa wa Manchester City na England, James Trafford, 23.
Hata hivyo, kwa asilimia kubwa, Newcastle inamtazama sana Trafford kwa sababu hatosumbua kuzoea mazingira kwani anaifahamu vizuri ligi hiyo.
Hidemasa Morita
LEEDS United imeanza tena mchakato wa kutaka kumsajili kiungo mkabaji wa Japan, Hidemasa Morita, 30, kutoka Sporting CP.
Inaelezwa Morita yuko tayari kujiunga na Leeds iwapo klabu hiyo itahakikisha inabaki kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.
Licha ya umri unaenda kumtupa mkono, Morita ana uzoefu wa kutosha ambao ndio umewapagawisha mabosi wa Leeds ambao wanaamini utaongeza kitu katika kikosi chao.
Mason Greenwood
MARSEILLE inaweza kulazimika kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa England, Mason Greenwood, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kutokana na changamoto za kifedha.
Inaelezwa Marseille inaamini ikimuuza Greenwood itapata pesa ambazo kwa kiasi kikubwa zitawasaidia kufukia mashimo ambayo wanayo kwa sasa.
Juventus inatajwa ni miongoni mwa timu ambazo zipo tayari kumsajili staa huyo ikiwa atawekwa sokoni. Marseille inadaiwa kuhitaji walau Euro 50 milioni kama ada ya usajili ya fundi huyo ambaye ina mkataba nao hadi mwaka 2029.
Richard Rios
MANCHESTER United imefikia hatua nzuri katika harakati zao za kumfuatilia kiungo wa Benfica na timu ya taifa ya Colombia, Richard Ríos, 25, ambaye inamhitaji akawe mbadala wa Casemiro anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu.
Awali ilielezwa huenda Benfica wakawa wagumu kumwachia fundi huyo kirahisi kutokana na umuhimu wake kwenye kikosi chao.
Rios ambaye msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Lucas Bergvall
KIUNGO wa Tottenham na Sweden, Lucas Bergvall, 20, anawindwa na Arsenal na Chelsea ambazo zinahitaji kumsajili dirisha lijalo.
Arsenal na Chelsea zinatamani sana huduma ya fundi huyu kwa ajili ya kuimarisha safu zao za kiungo ambazo wanaamini zina mapungufu.
Ripoti zinadai Spurs haitaki kumwachia kirahisi na Bergvall pia anasuburi kuona ikiwa Spurs itabakia katika ligi au laa kabla ya kufanya uamuzi.