Arsenal yakomaa na Barcola
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alianza katika kikosi cha Ufaransa kilichocheza dhidi ya Sweden Jumanne usiku, huku wajumbe wa Arsenal wakishuhudia mechi hiyo moja kwa moja.
LONDON, England: ARSENAL ipo tayari kujaribu kuishawishi Paris Saint-Germain (PSG) kumuuza mshambuliaji wake Bradley Barcola.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alianza katika kikosi cha Ufaransa kilichocheza dhidi ya Sweden Jumanne usiku, huku wajumbe wa Arsenal wakishuhudia mechi hiyo moja kwa moja. Barcola amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu na mabingwa hao wa Ligi Kuu England, sambamba na Morgan Rogers wa Aston Villa.
PSG kwa sasa ipo katika mbio za kusaka saini ya Yan Diomande kutoka RB Leipzig na Maghnes Akliouche wa Monaco, lakini haina mpango wa kumuuza Barcola.
Klabu hiyo tayari inamuuza Kang-in Lee kwenda Atletico Madrid, imemuuza Goncalo Ramos kwenda AC Milan, na inaendelea na mazungumzo na Juventus kuhusu kuondoka kwa Randal Kolo Muani.
Mauzo hayo yameipa PSG nafasi nzuri kifedha ya kuwasajili Diomande na Akliouche bila kulazimika kumuuza Barcola. Hata hivyo, klabu hiyo pia inahitaji kuongeza beki wa kati.
Barcola bado hajafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake. Kwa sasa hana hamu ya kuongeza mkataba mpya, huku akifahamu kuwa Liverpool pia ina nia kubwa ya kumsajili.
Kwa upande mwingine, Arsenal pia imejadili uwezekano wa kumsajili Morgan Rogers kutoka Aston Villa, lakini Villa haitaki kumuuza na inaaminika itahitaji ada ya uhamisho inayoweza kuvunja rekodi ya uhamisho nchini England endapo italazimika kufanya hivyo.
Vilevile, PSG itahitaji kiasi kikubwa cha fedha kwa Barcola ikiwa mchezaji huyo ataamua kushinikiza kuondoka.
Chini ya mkurugenzi mpya wa michezo Andrea Berta, Arsenal imekuwa ikifanya mazungumzo ya usajili wa wachezaji kadhaa kwa wakati mmoja hadi pale moja ya mikataba inapofanikiwa kukamilika.
Mfano wa mbinu hiyo ni kwamba Arsenal imetoa ofa kwa Bruno Guimaraes wa Newcastle United, huku pia ikiulizia uwezekano wa kumsajili Alex Scott wa Bournemouth.
Aidha, Arsenal imepewa nafasi ya kumsajili winga wa Club Brugge, Christos Tzolis, na pia imezungumza na wawakilishi wa kiungo wa Bayer Leverkusen, Kerim Alajbegovic.
Arsenal inalenga kusajili takribani wachezaji wanne wapya katika dirisha hili la usajili, lakini wote wanapaswa kuwa na kiwango cha juu.
Barcola anaonekana kutimiza vigezo hivyo, na Arsenal inaamini kuwa mchezaji huyo angependa kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo, haitakuwa pekee inayowania saini yake kwani klabu nyingine kubwa pia zinaendelea kumfuatilia.