Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ile ishu ya Rashford, Barcelona bado kizungumkuti

FUNUNU Pict

Muktasari:

  • Man United imegoma kabisa kushusha bei ya fundi huyu na mara kadhaa imesisitiza kama Barca itashindwa kulipa kiasi hicho cha pesa haitowauzia Rashford.

BARCELONA bado haijafanya uamuzi juu ya kulipa Euro 30 milioni ili kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United na  England, Marcus Rashford, 28.

Rashford, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Barca, amelivutia sana benchi la ufundi la  Barcelona tangu ajiunge nao kwa mkopo hali iliyosababisha wapendekeze asajiliwe mazima.

Hata hivyo, Barca inakumbana na kikwazo kikubwa katika kulipa kiasi cha pesa cha Euro 30 milioni kinachohitajika ili kumsainisha mkataba wa kudumu fundi huyo.

Man United imegoma kabisa kushusha bei ya fundi huyu na mara kadhaa imesisitiza kama Barca itashindwa kulipa kiasi hicho cha pesa haitowauzia Rashford.

Kuna uwezekano mkubwa pia staa huyu akauzwa kwenda PSG ambayo imeonyesha nia ya kumsajili na ipo tayari kutoa zaidi ya Euro 30 milioni ili kukamilisha usajili wake.

Barca inadaiwa pia kuomba kuipata huduma ya Rashford kwa mkopo wa msimu mmoja zaidi lakini Man United imekataa na kusisitiza namna pekee ya fundi huyo kurudi tena Nou Camp ni kwa kuuzwa.

Mkataba wa staa huyu na Man United unamalizika mwaka 2028.


Dusan Vlahovic

AC Milan imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Serbia, Dusan Vlahovic, 26, ambaye mkataba wake na Juventus unamalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Kumalizika kwa mkataba wake mwisho wa msimu huu  kumemfanya VlahoviC kuwa miongoni mwa wachezaji wanawaniwa na klabu nyingi Ulaya.

Vlahovic pia anawindwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu England ikiwemo Arsenal. Msimu huu amefunga mabao tisa ya Serie A.


Neymar Jr

FC Cincinnati ya Marekani inadaiwa kufikia hatua nzuri katika mazungumzo yao na wawakilishi wa mshambuliaji wa Santos, Mbrazil, Neymar Jr., 34, ambaye inataka kumsajili baada ya michuano ya Kombe la Dunia.

Inaelezwa  mazungumzo ya awali yamefikia hatua nzuri na Cincinnati inamwangalia Neymar kama mchezaji atakeyesaidia sana timu yao katika upande wa mvuto na kibiashara. Hata hivyo, Neymar amekuwa katika nyakati ngumu za majeraha.


Robin Roefs

CHELSEA imeanza mchakato wa kutaka kumsajili kipa wa Sunderland, Robin Roefs, 23, ili akawe mbadala wa kipa wa sasa, Robert Sanchez ambaye amekuwa akifanya makosa ya mara kwa mara yanayoigharimu timu.

Roefs ni moja ya nguzo muhimu Sunderland na amekuwa katika mwenendo mzuri msimu licha ya kuwa ndio imepanda daraja.

Sanchez amekuwa akihusishwa kuondoka tangu mwaka jana, sababu ikitajwa ni benchi la ufundi kutokuwa na imani naye.


Luka Vuskovic

BEKI wa Tottenham, Luka Vuskovic, 19, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Hamburger SV, anatarajiwa kurejea katika klabu hiyo msimu ujao baada ya kiwango chake kuimarika akiwa huko Ujerumani.

Awali, uongozi wa Spurs ulikuwa unafikiria kumuuza staa, lakini Vuskovic amezidi kuonyesha kiwango bora siku hadi siku kiasi cha kuwafanya vigogo hao wasitishe mpango wao. Beki huyo pia ana ofa kutoka kwa timu kadhaa Ulaya.


Jhon Lucumi

BEKI wa Bologna na  Colombia, Jhon Lucumi, 27, anaonekana kuwa karibu kuondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Inaelezwa Sunderland  bado inaonyesha nia ya kumsajili beki huyo, baada ya kushindwa kumpata katika jaribio lao la awali miezi kadhaa  iliyopita.

Lucumi ndio beki kiongozi wa safu ya ulinzi ya Bologna , lakini amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara. Msimu huu amecheza mechi 35 za michuano yote.


Christian Kofane

ARSENAL inatarajia kuwasilisha ofa Bayer 04 Leverkusen ili kumsajili mshambuliaji kijana wa klabu hiyo na Cameroon, Christian Kofane, 19.

Inaelezwa Leverkusen inahitaji hadi Pauni 60 milioni ili kumuuza mchezaji huyo dirisha la majira ya kiangazi.

Kofane kwa sasa ni mmoja wa mastaa tegemeo kikosi cha kwanza cha Leverkusen na mkataba wake unamalizika mwaka 2029.


Yan Diomande

MANCHESTER United na Liverpool zinaendelea kupigana vikumbo kuiwania saini ya winga wa RB Leipzig na timu ya taifa ya  Ivory Coast, Yan Diomande, 19.

Diomande ni miongoni mwa mastaa wanaokuja kwa kasi na timu hizo mbili zimekuwa zikimfuatilia kwa muda sasa na zinaona ni wakati sahihi kuwasilisha ofa katika dirisha lijalo. Mkataba wa sasa wa Diomande unamalizika mwaka 2030.