Liverpool, Iraola ni suala la muda tu
Muktasari:
- Iraola aliondoka AFC Bournemouth mwishoni mwa msimu na amekuwa akitajwa kama mgombea mkuu wa nafasi hiyo ndani ya viwanja vya Anfield.
LONDON, England: LIVEROOL imefikia makubaliano ya awali ya maneno na kocha Andoni Iraola ili awe kocha mkuu mpya wa klabu hiyo kufuatia kufutwa kazi kwa Arne Slot.
Iraola aliondoka AFC Bournemouth mwishoni mwa msimu na amekuwa akitajwa kama mgombea mkuu wa nafasi hiyo ndani ya viwanja vya Anfield.
Kwa mujibu wa ripoti ya The Athletic, Iraola anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 43 amekuwa akipendelea mikataba ya muda mfupi katika kazi yake ya ukocha akiwa na AEK Larnaca, CD Mirandes, Rayo Vallecano na Bournemouth.
Tangazo rasmi la kuthibitisha uteuzi wake linatarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa.
Mhispania huyo ana nia ya kwenda Anfield akiwa na wasaidizi wake wa Bournemouth, Tommy Elphick na Shaun Cooper, kama sehemu ya benchi lake la ufundi.
Taarifa imeeleza kuwa Bournemouth bado hawajapokea mawasiliano rasmi kutoka kwa Elphick au Cooper kuhusu mustakabali wao.
Liverpool wanataka kumteua kocha mpya haraka iwezekanavyo na wanatafuta mtu anayelingana na falsafa yao ya soka la kushambulia, lenye kasi na presha kubwa kwa wapinzani.
Inaelezwa pia kuwa Elphick, ambaye ni shabiki wa muda mrefu wa Liverpool, bado hajawasiliana na klabu hiyo, lakini angevutiwa na nafasi hiyo ikiwa itatolewa.
Beki huyo wa zamani wa Bournemouth mwenye umri wa miaka 38 alikataa nafasi ya kuwa meneja wa Bristol City wiki iliyopita ili apate muda wa kutathmini chaguo zake nyingine.
Mchakato wa kumtafuta kocha mpya Anfield unasimamiwa na mkurugenzi wa michezo wa Liverpool, Richard Hughes, ambaye aliwahi kufanya kazi na Iraola akiwa Bournemouth.
Liverpool walimfuta kazi Slot hivi karibuni ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kocha huyo Mholanzi kuiongoza klabu kutwaa taji la Ligi Kuu England.