Pedro kuziba pengo la Lewandowski Barcelona
Muktasari:
- Taarifa zinadai Barcelona inatafuta straika na imevutiwa zaidi na Pedro kutokana na umri wake, hivyo inaamini ikimsajili itamtumia kwa muda mrefu. Awali, Marcus Rashford ambaye anaichezea Barca kwa mkopo msimu huu alidaiwa kuwa mbadala wa Lewandowski, lakini mchakato wa kumsainisha mkataba wa moja unaonekana kuwa mgumu kutokana na kiasi cha pesa ambacho Man United inakitaka.
BARCELONA inamtazama mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil, Joao Pedro, 24, kama mmoja kati ya mastaa inaotaka kuwasajili ili kuziba nafasi ya straika Robert Lewandowski mwenye umri wa miaka 37 anayetarajiwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa zinadai Barcelona inatafuta straika na imevutiwa zaidi na Pedro kutokana na umri wake, hivyo inaamini ikimsajili itamtumia kwa muda mrefu. Awali, Marcus Rashford ambaye anaichezea Barca kwa mkopo msimu huu alidaiwa kuwa mbadala wa Lewandowski, lakini mchakato wa kumsainisha mkataba wa moja unaonekana kuwa mgumu kutokana na kiasi cha pesa ambacho Man United inakitaka.
Katika dili la Pedro, kwa upande wa Chelsea hadi sasa hakuna majadiliano yaliyofanywa ingawa inaaminika kwamba dili hilo litatokea ikiwa tu, Barca itawasilisha mezani ofa nzuri jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kutokea kutokana na hali ya kiuchumi ya sasa ya wababe hao. Mkataba wa Pedro na Chelsea unatarajiwa kumalizika 2029.
Cristian Romero
BARCELONA inapanga kuelekeza nguvu kwa beki wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Argentina, Cristian Romero, 28, iwapo jitihada za kumsajili Alessandro Bastoni, 27, kutoka Inter Milan katika dirisha lijalo zitafeli.
Hata hivyo, taarifa zinadai kwamba kuipata huduma ya Romero kutoka Tottenham Hotspur haitakuwa rahisi, kwani ni mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi hicho ingawa ikiwa itashuka daraja nguvu ya kumzuia asiondoke itakuwa ndogo.
Ibrahim Mbaye
ASTON Villa inamfuatilia mshambuliaji chipukizi wa PSG na Senegal, Ibrahim Mbaye, 18, ili kumsajili katika dirisha hili. Villa inaangalia wachezaji vijana, ikilenga kujenga kikosi cha muda mrefu na kuleta mafanikio ya baadaye.
Mbaye ni mmoja wa nyota wanaotajwa kuwa na vipaji vikubwa ingawa amekuwa hapewi nafasi ya kutosha. Iwapo PSG itagoma kumuuza, Villa inaweza kuomba kumsajili kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua moja kwa moja.
Anthony Gordon
WINGA wa Newcastle United na England, Anthony Gordon, 25, yupo katika rada za Bayern Munich. Taarifa zinadai wawakilishi wa Gordon wamekuwa kwenye mawasiliano na Bayern kwa miezi kadhaa, huku kocha Vincent Kompany akitajwa kuridhia kusajiliwa kwake.
Gordon ambaye pia anahusishwa na baadhi ya vigogo vya England, anaweza kuuzwa kwa takribani Pauni 80 milioni.
Lois Openda
COVENTRY City iliyopanda Ligi Kuu England msimu ujao inajiandaa kuingia katika vita dhidi ya Leeds United ili kumsajili mshambuliaji wa RB Leipzig na Ubelgiji, Lois Openda, 26. Openda ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Juventus amekuwa akihusishwa na klabu hizo mbili baada ya kufichuka kuwa Juventus haina mpango wa kumsainisha mkataba wa moja kwa moja kwa sababu haijaridhishwa na kiwango alichoonyesha.
Bailey Rice
NOTTINGHAM Forest, Aston Villa na Crystal Palace zote zinapambana kumsajili kiungo chipukizi wa Rangers na Scotland, Bailey Rice, 19. Rice ambaye msimu huu hajaonyesha kiwango bora katika Ligi Kuu Scotland, amekuwa akifuatiliwa na maskauti wa timu hizo za England tangu mwanzo wa msimu huu. Rangers haina uwezo wa kumzuia kuondoka kwa sababu mkataba wake unamalizika mwisho wa Juni, mwaka huu.
James Trafford
ASTON Villa ipo tayari kuongeza kasi katika jitihada za kumsajili kipa wa Manchester City na England, James Trafford, 23, majira ya kiangazi. Villa inamuona Trafford kama mbadala wa muda mrefu wa kipa wa kimataifa wa Argentina, Emiliano Martínez, 33, anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu. Trafford amekuwa akihusishwa kuondoka Man City sababu hachezo mara kwa mara.
Abde Ezzalzouli
LIVERPOOL imefikia hatua nzuri katika mchakato wa kumsajili winga wa Real Betis na Morocco, Abde Ezzalzouli, 24 ambapo ipo tayari kulipa Euro 60 milioni. Ezzalzouli ameonyesha kiwango bora msimu huu La Liga ambapo amefunga mabao 12 katika mechi 38 za michuano yote. Liverpool inamtazama kama nyongeza ya kuimarisha safu ya ushambuliaji kuelekea msimu ujao. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029.