Wakala wa Lewandowski akutana na Juventus
Muktasari:
- Lewandowski anabaki kuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani kutokana na uzoefu wake na hadi sasa haijajulikana ikiwa Barca itakubali aondoke mwisho wa msimu.
WAKALA wa mshambuliaji wa Poland, Robert Lewandowski, 37, anayekipiga Barcelona, anatarajiwa kukutana na Juventus wiki hii kujadili uwezekano wa staa huyo kutua katika klabu hiyo.
Wakati huo huo, AC Milan pia imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo mkongwe, ambaye bado anaendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao licha ya umri wake.
Lewandowski anabaki kuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani kutokana na uzoefu wake na hadi sasa haijajulikana ikiwa Barca itakubali aondoke mwisho wa msimu.
Mkataba wa sasa wa Lewandowski unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa haijajulikana ikiwa Barca itakuwa tayari kuona akiondoka katika kikosi chao.
Awali ilidaiwa kwamba angeruhusiwa kuondoka bure ili nafasi yake atakayoiacha izibwe na Marcus Rashford ambaye ameonyesha kiwango bora akiwa kwa mkopo katika kikosi chao msimu huu.
Inaelezwa ikiwa ataondoka Barca, kwa asilimia kubwa anaweza kutimkia Italia na sio Saudi Arabia kama ilivyowahi kubainishwa hapo awali.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Lewandowski amecheza mechi 40 za michuano yote na kufunga mabao 17.
Lucas Bergvall
KIUNGO wa Tottenham Hotspur na Sweden, Lucas Bergvall, 20, yupo katika rada za klabu kadhaa barani Ulaya baada ya kuvutiwa sana na kiwango chake.
Miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kwa karibu fundi huyu ni Arsenal na Chelsea , ambazo zinapambana kuimarisha maeneo yao ya kiungo.
Licha ya vigogo hao kuonyesha nia ya kumsajili, ripoti zinadai Spurs haitaki kumwachia kirahisi ingawa itashindwa kupambania kumbakisha ikiwa itashuka daraja.
Gabriel Martinelli
MSHAURI wa michezo wa Paris Saint-Germain., Luis Campos, ameripotiwa kufanya mazungumzo na wawakilishi wa winga wa Arsenal, Gabriel Martinelli mwenye umri wa miaka 24, pamoja na winga chipukizi wa RB Leipzig, Yan Diomandé, 19.
PSG wanaonekana kuendelea na mkakati wao wa kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kuchanganya mastaa wenye uzoefu na vijana.
Martinelli ni miongoni mwa mchezaji muhimu wa Arsenal sawa na ilivyokuwa kwa Diomande ndani ya Leipzig.
Eli Junior Kroupi
Bournemouth ipo tayari kumuuza mshambuliaji wake chipukizi wa kimataifa wa Ufaransa, Eli Junior Kroupi, 19, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Manchester United ni miongoni mwa klabu zinazomtamani nyota huyo, ambaye ameonyesha kiwango bora sana.
Ripoti zinadai Bournemouth inahitaji takribani Pauni 50 miolioni ili kumuuza Kroupi ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Ladislav Krejci
BEKI wa Wolves na Jamhuri ya Czech, Ladislav Krejci, ambaye alitimiza miaka 27 Jumatatu, yupo katika rada za Leeds United inayohitaji kumsajili kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Leeds inataka kuimarisha safu yao ya ulinzi baada ya kuona upungufu mkubwa tangu kuanza kwa msimu huu, hususani katika eneo la beki wa kati.
Krejci ana uwezo mkubwa wa matumivi ya nguvu na licha ya Wolves kufanya vibaya msimu huu, Krejci ameendelea kuonyesha kiwango bora.
Leo Scienza
SOUTHAMPTON ina imani kubwa ya kumbakisha winga wao wa kimataifa wa Brazil, Leo Scienza, 27, licha ya timu kadhaa kuonyesha nia ya kumsajili ikiwemo Leeds United.
Southampton inamwangalia Scienza kama sehemu muhimu ya mipango yao ya kikosi, hasa kutokana na mchango wake katika safu ya ushambuliaji msimu huu.
Leeds ipo tayari kutoa hadi Pauni 20 milioni kuhakikisha inaipata saini ya fundi huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Andreas Christensen
BEKI wa kimataifa wa Denmark, Andreas Christensen, 30, ameripotiwa kukataa ofa ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kusalia Barcelona. Hata hivyo, licha ya kukataa ofa hiyo, Christensen bado ana matumaini ya kuendelea kubaki ndani ya klabu hiyo, jambo linaloonyesha kuwa mazungumzo yanaweza kuendelea.
Beki huyo amekataa ofa hiyo kwa sababu ni ndogo tofauti na mahitaji yake rasmi. Mkataba wa fundi huyu unamalizika mwisho wa msimu huu.
Jacobo Ramon
BEKI wa kati wa Como ya Italia, Jacobo Ramon, 21, anatajwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kutua Arsenal katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Ramon anatajwa kuwa anatazamwa na maskauti wa timu nyingi tangu kuanza kwa msimu huu hali inayoongeza ushindani wa kuwania saini yake kwa sababu wengi wameonekana kuvutiwa na maendeleo yake.
Mbali ya Arsenal, Chelsea pia inahitaji huduma yake. Mkataba wa sasa wa Ramon unatarajiwa kumalizika mwaka 2030. Msimu huu amecheza mechi 31 za michuano yote.